Unordered List

Pages

Wednesday, November 28, 2012

Wabunge wa Kigoma wamtunishia misuli RC

Wabunge wa Mkoa wa Kigoma wamemtunishia misuli Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Mstaafu Issa Machibya, kutokana na kuwatishia kuwafunga pingu kama raia wengine wa kawaida, wakisema kauli hiyo ni dharau kubwa kwao wakiwa ni moja ya mihimili mitatu ya dola wenye jukumu la kuishauri na kuisimamia serikali, hivyo anapaswa kuwaomba radhi.
Kanali Machibya anadaiwa kutoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika kongamano la uwekezaji Kanda ya Ziwa Tanganyika, mkoani Katavi, kwa kutamka kwamba, mbunge yeyote atakayekaidi maelekezo yake au maelekezo ya mkuu wa wilaya atakamatwa na kupigwa pingu kama raia wengine wa kawaida.
Wakuu wa mikoa mitatu inayounda ukanda huo, ambayo ni Kigoma, Katavi na Rukwa, walihudhuria kongamano hilo pamoja na wakuu wa wilaya na watendaji wengine, wakiwamo makatibu tawala wa mikoa (RAS)na wilaya (DAS).

MOSES MACHALI
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alisema jana kuwa kwa kauli hiyo, Kanali Machibya ameonyesha kuwadharau wabunge kwamba, ni watu wasiofikiria.
“Kwa hiyo, tunamtaka ombe radhi. Aelewe kwamba, tunafanya kazi zetu kwa mujibu wa sheria. Hivyo, anapaswa aheshimu mhimili wa wabunge,” alisema Machali.
Alisema kauli hiyo ya Machibya ni ya kipuuzi na pia ni ya kifedhuli uliopindukia kwani imeonyesha mkuu huyo wa mkoa ana uwezo mdogo wa kufikiri kinyume cha ulimwengu wa sasa ulivyo.
Machali alisema Machibya anasahau kuwa yeye si bosi wa wabunge na kwa hiyo, hawezi kumfunga mbunge yeyote pingu kama anavyotamba.
Alisema kama itatokea mbunge akampinga mkuu wa mkoa, basi atakuwa ana sababu za msingi za kufanya hivyo.

Thursday, November 22, 2012

SEHEMU YA PILI: Mahojiano ya moja kwa moja na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe katika JamiiForums


MHOJAJI: Mkuu Zitto nashukuru kwa majibu yako kina kwa swali la kwanza, swali linalofuata;

B. Zitto na CHADEMA

1) Nini kipaumbele chako cha sasa kama mwanachama wa CHADEMA?

2) Mkuu, ni kweli kuwa CHADEMA ni chama cha kidini/kikabila? Na kama ni kweli, tatizo hilo lishughulikiwe vipi? Kama si kweli, unaweza kuueleza umma wa watanzania una kauli gani juu ya mitizamo hii dhidi ya chama chenu?

3) Mh. Zitto, unaizungumziaje demokrasia ndani ya chama chako katika chaguzi, teuzi na kupanga safu za uongozi?

4) Kwanini CHADEMA haiwatumii viongozi wa Mikoa na Wilaya na badala yake inatuma watu toka makao makuu hata kwa mambo madogo madogo ambayo yangemalizwa na uongozi wa ngazi husika?

5) Mh Zitto, unazizungumziaje harakati za M4C na athari (impact) yake kisiasa na kijamii? Chama kimeweka taratibu gani nzuri za malezi kwa wanachama wapya wanaojiunga kwenye M4C, kama bado, huku si kusuka kamba inayoungua?

6) Inadaiwa hushiriki kikamilifu M4C, ni kweli? Nini kauli yako dhidi ya tuhuma hizi?

7) Je, utaratibu wa kupita mikoani katika kutafuta nafasi ya kugombea uenyekiti kama ilivyokuwa wakati wa Mbowe unafaa au CHADEMA irudi katika utaratibu kama wa CCM?

8) Mhe. Zitto, Viongozi/CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kufichua ufisadi. Kuna taarifa kuwa kuna mwanachama wenu katafuna fedha za M4C, ni kweli? Kama ni kweli, ameshughulikiwaje? Kama hajashughulikiwa, ni kwanini mko kimya?

9) Zitto wewe ni naibu katibu mkuu wa CHADEMA, Mara nyingi matamko ya chama yametolewa na Katibu, Mwenyekiti, Mnyika (tangu kabla hajawa msemaji) na mara chache wanasheria km Lissu, Marando na Prof.Safari. Kwanini Zitto umekuwa mbali sana na matamko haya ya CHADEMA ukiwa kama Naibu Katibu mkuu? (Naamini hutojibu ni mgawanyo wa kazi)

10) Unafikiri CHADEMA uliyoikuta mwanzo ndiyo hii ya sasa au kuna mabadiliko? Kama kuna mabadiliko ni yepi na unafanya nini kufanya CHADEMA iwe kama ambavyo ulitaka iwe?

11) Unafikiri namna CHADEMA inavyoendesha siasa zake kuna uwezekano wa kushika dola mapema (2015)? Kama ndiyo kwanini na kama hapana unafikiri mabadiliko gani yanatakiwa kufanyika kuelekea 2015?

12) CCM wanadai kuwa nyinyi CHADEMA hamna presidential materials, una kauli gani juu ya hili?

13) Una muono gani kuhusu upinzani nchini na nini nafasi ya upinzani hasa CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ukilinganisha na chama tawala CCM?

ZITTO: Nitajibu tena kidogo kidogo maana hii peke yake ina maswali 13. 
1.Nini kipaumbele chako cha sasa kama mwanachama wa CHADEMA? 
 
 - Kutumikia chama chetu kwa nafasi nilizonazo.

Natumia nafasi yangu ya Ubunge na Uwaziri kivuli kuhakikisha kuwa chama kinapata taswira chanya mbele ya jamii, Na kinaleta mabadiliko ambayo chama tawala, yaani CCM, kinashindwa kuwafikishia wananchi. Utaona kwamba, kama unafuatilia Bunge, hakuna mkutano wa Bunge unaopita bila hoja mahususi inayojenga taswira chanya ya chama.

Ni bahati mbaya sana kuwa hatutumii baadhi ya mafanikio yetu Bungeni kwenye ulingo wa siasa ma hivyo kuwaacha CCM wanachukua credits.

Kwa mfano, ni kwanini mafanikio ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu hatujayafanyia kazi ya kisiasa? Ingawa hatukufanikiwa kumtoa Waziri Mkuu lakini tuliilazimisha Serikali kufanya mabadiliko. Kikwete alisema ni upepo tu, lakini upepo huu ulikuwa na joto kali ukamshinda na tukaacha yeye achukue credit kwa kazi yetu ya uwajibikaji.

Hoja ya juzi ya Mheshimiwa Halima Mdee kuhusu Ardhi inabidi kuifanya ni ajenda ya kisiasa. Hoja ya Mkonge tulikwenda Tanga na ilikuwa na mafanikio makubwa sana. Hoja ya Mabilioni ya Uswiss nayo tunaiachia wanaisemea watu wa CCM kuififiza. Historia inatuonyesha kuwa hoja zote tulizozitumia vizuri nje ya Bunge zilijenga taswira nzuri ya chama ie Buzwagi na EPA. We ignore this at our own peril
 
2.Mkuu, ni kweli kuwa CHADEMA ni chama cha kidini/kikabila? Na kama ni kweli, tatizo hilo lishughulikiwe vipi? Kama si kweli, unaweza kuueleza umma wa watanzania una kauli gani juu ya mitizamo hii dhidi ya chama chenu?
 
- Chadema ni chama cha kitaifa. Kingekuwa chama cha kidini au kikabila kingefutwa. Katika uongozi wa Chadema unapata watu toka mikoa na kabila mbali mbali, pia watu toka dini mbali mbali. Diversity hii haipatikani katika vyama vingi humu nchini. Nadhani mtazamo huu unapandikizwa na watu ambao hawakipendi chama chetu na wanao ona chama kama threat kwa maslahi yao binafsi.

Pia sisi kama chama tunapaswa kuwa makini sana, hasa viongozi tunapofanya kazi zetu ili kutothibitisha taswira hii mbaya dhidi ya chama chetu. Baadhi ya wanachama wa CHADEMA ndio mabingwa wa kueneza jambo hili. CCM nao humo humo wanapandikiza mbegu za chuki. Unakuta Waziri wa CCM anamwita Mbunge wa CHADEMA na kumwambia, fulani bwana mdini sana. Mwangalieni. Kiongozi wa CHADEMA anajiona kapata bonge ya issue na kueneza. Tunachinjwa na CCM kwa upuuzi wetu. Kwa ujinga wetu wenyewe. Chama chetu kimesambaa nchi nzima na viongozi wake ni wa dini zote na makabila yote.

3.Mh. Zitto, unaizungumziaje demokrasia ndani ya chama chako katika chaguzi, teuzi na kupanga safu za uongozi?
 
CHADEMA ina demokrasia ya aina yake na wanachama tunaridhika nayo. The Party deploys for or against your wishes and every member must oblige a just deployment. Tuna utaratibu mzuri sana wa kujieleza na kutetea hoja zetu ndani ya chama, na baada ya watu wote kukubaliana tuna hakukusha tunasimama wote kwa kauli moja sehem zote tunapo wakilisha chama. Sio katika kupanga safu za uongozi tu, ni sehem zote za uongozi wa chama.

4.Kwanini CHADEMA haiwatumii viongozi wa Mikoa na Wilaya na badala yake inatuma watu toka makao makuu hata kwa mambo madogo madogo ambayo yangemalizwa na uongozi wa ngazi husika?
 
Huo mtazamo unaweza kutokana na kulinganisha Chadema na vyama vingine. Ieleweke kua Chadema ni chama tofauti na kina utaratibu wake. Katika chama chetu Viongozi wa mikoa na wa wilaya wana majukumu yao, na makao makuu pia yana majukumu yake.

Inaweza kutokea mara kwa mara hizi level mbili zishirikiane katika kutekeleza kazi za chama. Hata hivo, tunaendelea kujenga chama kama taasisi, hivyo tunaendelea kujenga uwezo wa viongozi wetu wa mikoa na wilaya ili waweze kumudu majukumu mengi zaidi na kuwaachia wenye kukaa makao makuu kuhusika zaidi na strategies za chama.
5.Mh Zitto, unazizungumziaje harakati za M4C na athari (impact) yake kisiasa na kijamii? Chama kimeweka taratibu gani nzuri za malezi kwa wanachama wapya wanaojiunga kwenye M4C, kama bado, huku si kusuka kamba inayoungua?
 
Kwa sababu jina lake liko wazi kabisa, M4C ni moja ya operesheni inayo fanikisha watanzania kujiunga katika chama huku wakijua kabisa kua malengo ni kuleta mabadiliko chanya.

Impact yake kwa jamii ni kubwa sababu inawaweka wanachama wenyewe kua vyanzo vya mabadiliko. Baada ya kujiunga, ni obvious kua Chama kinatoa mafunzo kwa wanachama wake wapya na hivyo kuwalea kuwa makada wazuri. Hii sio opresheni ya kwanza ya Chama, na haitakua ya mwisho.

M4C sio chama ndani ya chama, M4C ni operesheni ya kujenga chama na kuleta mabadiliko nchini.
 
6.Inadaiwa hushiriki kikamilifu M4C, ni kweli? Nini kauli yako dhidi ya tuhuma hizi? 
 
 Ninashiriki sana kazi za kujenga chama. Nimeshiriki sana operesheni mbalimbali za chama. Nitaendelea kushiriki nikiwa mwanachama na kiongozi wa chama.

Halikadhalika wengine tunashughulika zaidi katika kuwakilisha chama Bungeni na mikakati mengine ya kuhimarisha chama, ila tukipata nafasi tunajiunga pia katika kazi za kujenga chama. Mikutano yetu ya chama tunagawana maeneo.

Mimi, kwa mfano kwenye M4C nimepangiwa mkoa wa Manayara na Singida nikiwa na Tundu Lissu na Christina Lissu na Rose Kamili. Mtakumbuka mwanzo mwa mwaka nilifanya ziara Tanga bila viongozi wenzangu. Mtakumbuka nilikwenda Marekani kufungua tawi la chama kule. Nimefanya mikutano Iringa, Hanang nk. Nimeshiriki kampeni za udiwani maeneo mbalimbali nchini. Siwezi kuonekana kila mkoa kila wakati. Pia ninapangiwa kazi.
 
7.Je, utaratibu wa kupita mikoani katika kutafuta nafasi ya kugombea uenyekiti kama ilivyokuwa wakati wa Mbowe unafaa au CHADEMA irudi katika utaratibu kama wa CCM?
 
Hatujawahi kufanya utaratibu unaosema isipokuwa kwenye Urais mwaka 2005. Hatujarejea tena utaratibu huo. Mfumo wowote ambao unapanua demokrasia ya chama ni bora zaidi katika kuimarisha chama. Chama kinakomaa kwa wanachama kushindana kwenye chaguzi za ndani. Natumai uchaguzi mkuu ujao wa chama utakuwa na wagombea wengi zaidi ili wanachama wapate uchaguzi wa kweli. Sipendi chaguzi za kupita bila kupingwa katika chama kinachotaka kujenga demokrasia ya nchi.

8.Mheshimiwa Zitto Viongozi/CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kufichua ufisadi. Kuna taarifa kuwa kuna mwanachama wenu katafuna fedha za M4C, ni kweli? Kama ni kweli, ameshughulikiwaje? Kama hajashughulikiwa, ni kwanini mko kimya?
 
Nasikia suala hili hapa, tupeni ushahidi na tutachukua hatua mara moja.

9.Zitto wewe ni naibu katibu mkuu wa CHADEMA, Mara nyingi matamko ya chama yametolewa na Katibu, Mwenyekiti, Mnyika (tangu kabla hajawa msemaji) na mara chache wanasheria km Lissu, Marando na Prof.Safari. Kwanini Zitto umekuwa mbali sana na matamko haya ya CHADEMA ukiwa kama Naibu Katibu mkuu? (Naamini hutojibu ni mgawanyo wa kazi)
 
Naibu Katibu Mkuu sio msemaji wa chama. Katika kujibu suala la demokrasia katika chama nilisema kuwa kuna utaratibu wa kujadili hoja mbali mbali ndani kwa ndani, yakiwemo matamko ya chama.

Katibu mkuu wa CHADEMA anapotoa matamko ya chama anatoa yale yaliyojadiliwa na wanachama wote, nikiwemo mimi, hivyo kuwakilisha maoni yangu pia. Sidhani kama kuna umuhimu wa kuifanya kazi hiyo wakati nimeridhika kua maoni yangu yanawakilishwa kupitia utaratibu wa chama.

10.Unafikiri CHADEMA uliyoikuta mwanzo ndiyo hii ya sasa au kuna mabadiliko? Kama kuna mabadiliko ni yepi na unafanya nini kufanya CHADEMA iwe kama ambavyo ulitaka iwe?
 
CHADEMA ni chama kinachokua kwa kasi sana, na kadiri kinavyokua kinabadilika positively. Moja ya mabadiliko hayo ni idadi ya wanachama, nyingine ni kuweza kushika Uongozi wa Upinzani Bungeni, nafasi ambayo ilikua ya CUF nilipo ingia chama. Chama hivi sasa kipo kila mahala.

Nakumbuka mwaka 2005 tulikwenda Mafinga kuhutubia tukapata watu 20 tu kwenye mkutano. Leo tunaombwa kwenda huko. Chama kina influence maamuzi ya nchi hivi sasa. Hayo yote ni mabadiliko makubwa na mazuri, na ninafurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya chama changu.

11.Unafikiri namna CHADEMA inavyoendesha siasa zake kuna uwezekano wa kushika dola mapema (2015)? Kama ndiyo kwanini na kama hapana unafikiri mabadiliko gani yanatakiwa kufanyika kuelekea 2015?
 
Sina mashaka na hili. Nitafafanua zaidi baadaye
 
12.CCM wanadai kuwa nyinyi CHADEMA hamna presidential materials, una kauli gani juu ya hili?
 
Kweli unategemea kuwa chama tawala kinaweza kukisifu chama cha upinzani kwa kuwa na presidential material? Mimi ni Presidential material kwa mfano.

Nina Uwezo, Uadilifu na Uzalendo wa kuweza kuwa Amiri Jeshi Mkuu. Dkt. Slaa ni Presidential Material. Mbowe ni Presidential material. Kitila Mkumbo ni Presidential material. Wapo wengi sana ndani ya CHADEMA wenye sifa za kuwa Marais. Sina mashaka kabisa hilo.

13.Una muono gani kuhusu upinzani nchini na nini nafasi ya upinzani hasa CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ukilinganisha na chama tawala CCM?
 
Ili Tanzania iwe salama ni lazima CCM ishindwe uchaguzi. CCM ikishinda tena mwaka 2015 itavunja sana moyo wa wananchi na wengine wanaweza kukata tama. Lakini pia CCM imechoka na haina nguvu za kutosha kukabiliana na changamoto za nchi hivi sasa.

Njia pekee ya kuisadia CCM iweze kujipanga upya ni yenyewe kondoka madarakani. CHADEMA ina nafasi kubwa sana ya kushinda na kuongoza dola. Muhimu chama kijipange na kuonekana kama chama kilichotayari kushika dola. Tuyatende tunayoyasema na tujiimarishe zaidi.
 
MWISHO WA SEHEMU YA PILI SUBIRI SEHEMU YA TATU

Wednesday, November 21, 2012

KAMA HUKUPATA NAFASI YA KUSOMA MAHOJIANO YA ZITTO KWENYE JAMII FORUM NAKULETEA MAHOJIANO YA AWALI

>>MASWALI NA MAJIBU YA ZITTO KABWE NA JF


 ZITTO:Re: Mahojiano ya moja kwa moja na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe katika JamiiForums

Awali ya yote itoe shukrani zangu za dhati kwa kupewa fursa hii adimu ya kuhojiwa na wana JF wenzangu.

Nashukuru pia kwa kuwa ni heshima kubwa sana kwangu maana mimi ni mtu wa pili kufanyiwa mahojiano kama haya baada ya kijana mwenzetu Maxence kama 'founder' wa jukwaa letu. Napenda pia ifahamike kuwa mimi ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa jukwaa hili na ninafurahi kuona limekuwa na kwa kweli its a force to reckon with.

Zitto ni Mtanzania aliyezaliwa Kigoma, Kijiji cha Mwandiga. Nimekulia katika kitongoji cha Mwanga, nimekwenda shule ya Msingi Kigoma, Sekondari Kigoma, Kibohehe Moshi, Galanos Tanga na Tosamaganga Iringa. Nimepata Elimu ya Juu Chuo Kikuu cha Zanzibar kwa mwaka mmoja, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Uchumi, Scholarship ya InWent Biashara ya kimataifa na Bucerius School of Law and Business Mineral Economics.

Ninaishi Kijijini Kibingo, Kata ya Mwandiga Wilaya ya Kigoma. Pia Tabata wilaya ya Ilala na Dodoma nyakati za Bunge. Ninaishi na mama yangu mzazi na wadogo zangu.

MHOJAJI:A. Zitto na Ombwe la itikadi miongoni mwa vyama vya siasa


Ni dhahiri CCM na Chadema sera zao ni zile zile katika mazingira ya soko huria, tofauti yao pengine ni ukosefu wa sheria zenye meno kudhibiti mambo Fulani Fulani, au mapungufu katika uwajibikaji, utekelezaji n.k; Kutokana na hili, ni vigumu kutofautisha kwa kina CCM ikulu 2015, hasa ile ambayo itaamka kutoka usingizini, na Chadema ikulu 2015 ambayo itapatikana pengine kutokana na vita dhidi ya ufisadi na pia ukali dhidi ya utekelezaji mbovu wa sera za CCM, usimamizi mbovu wa rasilimali za taifa, na tabia ya viongozi kutowajibika.

Hayana yote matatu hayana itikadi, na iwapo CCM itabadilika, Chadema itakuwa katika wakati mgumu kuendelea kuipa ushindani CCM; Ndio maana unakuta comments za Chadema kuhusu mabadiliko ya uongozi CCM etc ni za kuponda tu kwamba ‘hakuna kitakachobadilika’, kwani nje ya kusema hayo, hakuna hoja nyingine yenye mashiko kwani hoja ya ufisadi itapotea hivi hivi….

1. Unalizungumziaje Ombwe la Itikadi Miongoni mwa Vyama vyetu vya Siasa, ambapo tangia mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaingie nchini, ni vigumu kutofautisha itikadi za vyama vya siasa - kinadharia na kivitendo, hasa ukizingitia ukweli kwamba kwa kila chama, sera na itikadi zinazouzwa au kutekelezwa ni za kiliberali, huku wananchi wengi (hasa vijijini) wakiwa hawana ufahamu juu ya madhara na faida ya itikadi hii ni nini.

2. Unaiongeleaje sera ya Majimbo ya CHADEMA?

3. Unaona tofauti ya msingi kati ya CCM na CHADEMA ni IPI?

4. Nini kinakuvutia ndani ya CCM ambacho hakipo CHADEMA?

5. Bado unafikiri wewe kuwa CHADEMA ni tija kwa jamii kuliko kuwa Chama kingine mfano CCM?

6. Unalizungumziaje suala la kuwa na utitiri wa vyama vingi vya siasa vinavyokula pesa za walipa kodi halafu havina tija wala mchango wowote kijamii zaidi ya kutufilisi, je kuna umuhimu wa kuifanyia sheria mabadiliko ili kuwe na limitation mfano, vyama vitatu tu?


ZITTO:

Maswali marefu sana. Nitajibu kidogo kidogo.

1. Unalizungumziaje Ombwe la Itikadi Miongoni mwa Vyama vyetu vya Siasa, ambapo tangia mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaingie nchini, ni vigumu kutofautisha itikadi za vyama vya siasa - kinadharia na kivitendo, hasa ukizingitia ukweli kwamba kwa kila chama, sera na itikadi zinazouzwa au kutekelezwa ni za kiliberali, huku wananchi wengi (hasa vijijini) wakiwa hawana ufahamu juu ya madhara na faida ya itikadi hii ni nini.

- Hii ni changamoto kubwa sana kwa nchi yetu. Itikadi za kisiasa husaidia kunyoosha sera za vyama. Hivi sasa chama chochote chaweza kuwa na sera yeyote ile kwa kuwa hakuna uti wa mgongo ambao ni itikadi. Lazima vyama vijipambanue kwa itikadi zao. Kwa kukosekana kwa itikadi zinazoeleweka vyama vimekuwa kama 'electoral machines' tu. Kukosekana kwa itikadi kunafanya vyama kudandia masuala. Mfano juzi hapa mmesikia Mkutano Mkuu wa CCM umeazimia elimu iwe bure.

CHADEMA tulisema hivi mwaka 2010, CCM wakasema huo ni uwendawazimu kwani haiwezekani. Nakumbuka nilikuwa kwenye mdahalo pale Serena (hivi sasa) mwaka 2010, vijana wa CCM wakaniuliza mtapata wapi pesa za kusomesha watu bure. Nikawajibu kama tuliweza kuwasomesha bure kwa Tumbaku, Kahawa na Pamba, tutawasomesha bure kwa dhahabu, tanzanite nk. Leo CCM wanasema elimu bure. Nimemsikia Lowassa juzi anasema inawezekana. Lowassa huyu nilibishana naye sana mwaka 2010 akisema haiwezekani. Huu ni ukosefu wa itikadi sahihi.

Sababu kubwa pia viongozi wetu hawasomi na hivyo bongo zao hazipo 'sharp' kuweza kuona ni mwelekeo gani wa itikadi wa kufuata. At best tunaimba kama kasuku itikadi zilizoendelezwa nje, hakuna originality
2.Unaiongeleaje sera ya Majimbo ya CHADEMA? 
 - Ni utekelezaji wa kushusha madaraka mikoani, kupanua uwajibikaji na kuleta maendeleo kwa wananchi. Sera hii ya utawala ndio suluhisho la masuala mengi ya uwajibikaji hapa nchini. Kuna haja ya kuwa na DC? Kwa nini wakuu wa mikoa wasichaguliwe na wananchi? Tulipoamua kupendekeza sera hii kwa wananchi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 tuliambiwa sisi tuna lengo la kuleta ukabila nchini. Inawezekana kuna maeneo fulani fulani tulikosea mkakati. Kwa mfano tulianza kusemea suala hili tukiwa mkoani Kilimanjaro, kwa hiyo CCM ikadakia 'unaona wachaga hawa' sasa wanataka ka nchi kao. Kimkakati tulikosea.

Tulipaswa kuzindua sera hii kanda ya Ziwa au kanda ya Kusini. Tulijifunza kutokana na makosa haya. Hivi tumejiandaa vizuri zaidi kuielezea sera hii. Tunataka kuimarisha Halmashauri za Wilaya/Miji/Manispaa/Majiji kwa kuoondoa nafasi ya Wakuu wa Wilaya na kada nzima pale Wilayani. Majukumu yote ya kisiasa ya DC atayafanya Mwenyekiti wa Halmashauri. Majukumu yote ya Kiutendaji ya Ofisi ya DC atayafanya Mkurugenzi wa Halmashauri. Wakuu wa mikoa wachaguliwe na Wananchi moja kwa moja na wawe na 'executive powers' kwa mambo ya mkoa husika. Tutayaweka kisheria mambo haya. Hii mambo ya Rais kuteua wakuu wa Mikoa nchi nzima hapana. Watu wachaguliwe.

Ninaamini kabisa kuwa Sera hii ikitekelezwa tutaweza kutumia rasilimali zetu vizuri na mikoa itashindana kimaendeleo badala ya kushindana kwa namna walivyompokea Rais mkoani kwao

MAHOJIANO YA ZITTO KABWE LIVE MUDA HUU JAMII FORUM


Mahojiano ya moja kwa moja yameanza katika thread hii - Mahojiano ya moja kwa moja na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe katika JamiiForums

Na hivyo mnakaribishwa kufuatilia, thread hii ni kwa ajili ya side comments na ile ya mahojiano itaendeshwa na AshaDii na atakuwa anajibizana na Mhe. Zitto.



FUATILIA MAHOJIANO HAYO HAPA KWA KUBONYEZA LINK HII>>>>>>>>>>>>>>>>>>
 

Monday, November 19, 2012

J.K ni Jembe. ## MAKALA FUPI KUTOKA KWA MJENGA WA "JF"


Haina ubishi kuwa J. Kikwete ni rais pekee ametawala kwa mizengwe lakini namna anavyoipangua mizengwe hiyo, anastahili pongezi kubwa. Ikumbukwe zengwe la kwanza ni lile la kukataliwa na CHADEMA kuwa si rais halali, wakaenda mbali zaidi kwa wabunge wake kumzilia hotuba yake ya ufunguzi na kutoka nje ili kumdhalilisha, huku katibu mkuu kutangaza kuwa atahakikisha J.K hatawali.

Kikwete kwa umahiri mkubwa alitulia na kuendelea kuhutubia huku akiwahakikishia kuwa "ipo siku watarudi kwake" (walirudi hawakurudi?). Zengwe lingine ni la kudai kumshtaki J.K kwa wananchi ili kumshinikiza aondoke madarakani. Hili pia lilifanywa na CHADEMA kupitia maandamano sehemu mbalimbali za nchi wakilenga zaidi kutengeneza propaganda ya kuidanganya jumuiya ya kimataifa kuwa J.K hakubaliki na wananchi.

Hilo lilishindwa kwakuwa J.K alitulia na wala hakutaka kutumia nguvu ya dola ambao kimsingi ndiyo mtego ulikuwa umewekwa na CHADEMA. Maandamano yaliposhindwa, ukaanza ushawishi wa migomo kwa wafanyakazi walimu na madaktari, nalo lilishughulikiwa kwa umakini kila mtu anajua. Propaganda ya Ulimboka iliyoshikiwa bango na CHADEMA na wanaharakati kwa kumlazimisha Ulimboka aseme hata yasiyokuwepo, iligonga mwamba.

Zengwe zimezidi kuendelea kupitia M4C ya CHADEMA ambayo kwa mgongo wa elimu ya uraia ililenga kushawishi wananchi kuikataa serikali ya J.K kwa mtindo wa Libya, Tunisia na Misri, hiyo nayo nia wazi wananchi wameishtukia kuwa haina nia nzuri na hatma ya Amani ya Tanzania. Imekataliwa na ushahidi ni matokeo ya udiwani wa kata 29 uliofanyika hivi majuzi ambapo CHADEMA pamoja na nguvu kubwa ya M4C iliambulia kata 5! huku CCM ikijikombea kata 22 kati ya 29 zilizokuwa zinagombewa.

J.K amezidi kuimarisha CCM huku CHADEMA wakichelewa kugombania nani agombee urais/uenyekiti wa chama na kibaya zaidi na bila kujijua wote wamejikuta wanaimba wimbo wa CCM na kukiacha chama kikizidi kuangamia. Aliyozuiliwa Zitto kuyafanya, ndiyo yafanywayo na Mbowe.

Juzi juzi hivi Mbowe amesikika akiupongeza urais wa J.K na kukiri kuwa ni urais uliotukuka uliojaa busara na hekima na kwamba kwa TZ hakuna kama J.K. Kimsingi Slaa amejikuta akibaki peke yake aking'ang'ana na siasa za chuki na utovu wa nidhamu kwa J.K huku wenzake wote waliomzunguka wakimuasi bila yeye kujijua. J.K hajateteleka kiutendaji , zaidi ameendelea kukomaa na kujawa na maarifa zaidi.

Sote tumeshuhudia jinsi serikali ya awamu ya nne ilivyovunja rekodi kwa ujenzi wa miundo kupitia hotuba ya Magufuli wakati wa Mkutano mkuu wa CCM Dodoma.

Kwa hakika J.K ni rais ambaye amewabaini wabaya wake mapema na sasa anacheza nao kama atakavyo. Anajua pia wabaya hao bado wanamtafuta kwani bado hawajakidhi haja ya kiu yao ya kuona J.K akitolewa ikulu kwa madai ya kuushindwa Urais. J.K kweli ni zaidi ya "jembe".

SOURCE: JF

HII IMETOKA JAMII FORUM KAMA ILIVYO### Kauli tatu tata za mwenyekiti wa CHADEMA (Freeman Mbowe) ktk kipindi kisichozidi miezi 3 JE KUNA UKWELI WOWOTE

Kauli tatu tata za mwenyekiti wa CHADEMA (Freeman Mbowe) ktk kipindi kisichozidi miezi 3

WAKUU WANA-JF

Kwa kipindi kisicho zidi muda wa miezi mitatu(3) kumekuwa na lugha ama sentesi kadhaa kutoka kwa Mh. Freeman Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa CHADEMA taifa ambazo wachambuzi wa kisiasa kama sisi ni lazima tuzijadili kwa kina kwa sababu hatujawahi kuzisikia kutoka kinywani kwa Kiongozi huyu siku za nyuma pia ni haba sana kuzisikia hasa kwa CHAMA MAKINI KAMA CHADEMA katika taifa hili.

Mbowe akiwa kama nguzo imara ya upinzani na amekuwa na machngo mkubwa sana katika harakati za ukombozi ndani ya taifa hili,Lakini lugha zake za hivi karibuni zina ukakasi mkubwa sana pia ni tata kwa wananchi ambao wanaamini kabisa CHADEMA kinaweza kuwa chama mtambuka cha ukombozi ndani ya taifa hili.

KAULI TATA AMBAZO ZINAZUA MASWALI MENGI KUTOKA KWA MH:FREEMAN AIKAEL MBOWE NI HIZI
1. Kupitia gazeti la majira la wiki tatzu zilizopita Mh.Freeman mbowe alinukuliwa akisema Yupo tayari kuachana na chadema wakati wowote atakapo amua.

Kauli hii ni tata na mlengo wake unazua maswali mwengi sana.Tujiulize mbowe anasema kuwa anatakuacha na siasa za CHADEMA wakati wotete Je ni kwamba amechoka kupigana na CCM?Au ameshavuna mazao ya siasa na hahitaji tena kuendelea kuyala?Naweza kwenda mbali kabisa kwamba Mbowe anapotangaza kuachana na siasa za CHADEMA ni kwamba anataka kuudhihirishia umma kuwa CHADEMA si mali yake(familia) kama wengi wanavyokitafsili?

Lakini kauli kama hii mbowe haoni kama anakatisha tamaa kwa viajana ambao wamekuwa wakijiunga na CHADEMA kutokana na yeye kuwa mwanaharakati makini kwa muda mrefu?

2. Kupitia GAZETI LA TANZANIA DAIMA wiki iliyopita Mh.Mbowe alitangaza kumkaribisha waziri mkuu wa zamani Mh.Fredrick sumaye kwenye ulimwengu wa siasa za CHADEMA.

Swala hili hakika linazua maswali mengi sana.Ikumbukwe SUMAYE ni mmoja ya mafisadi papa wa nchi hii na alikuwemo kwenye LIST OF SHAME iliyosomwa na CHADEMA pale mwembe yanga.Je sumaye ameshakuwa msafi kiasi kwamba anapewa nafasi na CHADEMA?

Kelele za chadema siku zote ni kupingana na rushwa iweje leo mtuhumiwa mkubwa wa rushwa nchini kama sumaye aonekane muhimu mbele ya chadema na hatimaye kumtaka asajiliwe?

Lakini tuende mbali zaidi yawezekana MBOWE anamuita SUMAYE aje chadema kwa ile kauli ya WANYUMBANI NJOO NIKUSHIKE MKONO SIPO RADHI UFIE JANGWANI hatakama ni haramu??????.........ni siku chache sana SUMAYE amebwagwa kwenye uongozi ndani ya ccm na ameishia kulalama kuhusu kufanyiwa mchezo mchafu.

3. Kauli ya tatu tata zaidi ni ile aliyoitoa pale HAI alipokuwa anamkaribisha na kumshukuru Mh.Rais kikwete kwa utendaji wake.Mbowe alinukuliwa akisema"nimetembea angani na aridhini Tanzania nzima sijaona Rais na serikali iliyotukuka kiutendaji kama hii ya KIKWETE."

Nachelea kusema maneno hayahaya yangesemwa na chama chochote kingine yangezua gumzo,au yange semwa na mwanachadema yeyote yule yangezua mjadala mkubwa wakitaifa.

Naomba kuuliza hii ni kauli sahihi ya kiongozi wa upinzani kumwambia Rais wa nchi hata kama ana show appriciation ya kile kilichofanyika?Hakuna lugha nyingine yakipinzani-yakusifia ambayoingetumika hapa???



Mbowe huu ni wakati wakuwekana wazi kwa watanzania, KAMA UKOMBOZI UMESHAUZWA NI HERI WATANZANIA WAKAAMBIWA kuliko maneno kama haya ya kusifia kupitiliza as if nchi hii hakuna upinzani.
WANA-JF nawasilisha naomba tujadiliane kwa makini namna kauli hizi zinavyoathiri chama na zinavyojenga chama.

Wednesday, November 14, 2012

KIKWETE MWENYEKITI TENA CCM, MANGULA, DK, SHEIN MAKAMU WAKE

 
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akipongezwa na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Makamu wenyeviti wawili, Spika wa Bunge Anna Makinda, baada ya kumtangaza kushinda nafasi hiyo ya Uenyekiti, katika uchaguzi uliofanyika hivi punde katika ukumbi wa Kizota, Dodoma, ikiwa ni kuhitimisha shughuli za Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM. Wapili Kulia ni Makamu Mwenyekiti Mpya wa CCM (Zanzibar) Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais Dk. Moahamed Gharib Bilal
Mwenyekiti wa CCM, Taifa, Jakaya Kikwete na Makamu wake wawili Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (Zanzibar) na Philip Mangula (Bara) wakiwa meza kuu baada ya kutangazwa kushika nyandhifa zao.
Wajumbe wakiserebuka baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangazwa kuwa mshindi wa Uenyekiti wa CCM, Taifa.
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete akiongoza kikao baada ya kushinda tena kiti hicho. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Dk. Ali Mohamed Sheni na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phili Mangula.
 

NA HAPA CHINI NI MATOKEO YA UNEC

1. Stephen Wassira - 2,135
2. January Makamba – 2,093
3. Mwigulu Nchemba – 1,967
4. Martine Shigela – 1,824
5. William Lukuvi – 1,805
6. Bernard Membe – 1,455
7. Mathayo David Mathayo – 1,414
8. Jackson Msome - 1,207
9. Wilson Mukama - 1,174
10. Fenela Mukangara - 984
 
 
PICHA ZOTE NA CCM BLOG

HALMASHAURI KUU YA TAIFA YAFANYA UCHAGUZI WA WAJUMBE WA SEKRETARIETI YA HALMASHAURI KUU YA TAIFA.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) kimekutana katika Ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya chama, maarufu kama Whitehouse mjini Dodoma,leo tarehe 14th Nov 2012.

Kikao hicho kitajadili juu ya kuunda na kupitisha majina yaliyopendekezwa na Mwenyekiti wa ChaCha Mapinduzi Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama ya Taifa (CC) pamoja na uundaji wa sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa. Ambapo Mwenyekiti wa Chama kwa mujibu wa Kanuni na Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, anayo fursa ya kuteua wajumbe kumi(10) wa Halmashauri kuu ya Taifa, ambapo Mwenyekiti aliwateua wajumbe wanne(4) na akabakiza nafasi nyingine sita (6) miongoni mwa wajumbe hao ni Mhe. Asha-rose Migiro, Mhe. Zakhia Meghji, Mhe. Nape nnauye na Mhe. Abdulrahaman Kinana .
Baada ya uteuzi huo Mwenyekiti pia alipendekeza majina ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ambapo alipendekeza majina yafuatayo;
  1. Nafasi ya Katibu Mkuu, alimpendekeza Mhe. Abdulrahaman kinana.
  2. Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mhe. Vuai Ali Vuai.
  3. Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, Mhe. Lameck Madelu Nchemba.
  4. Katibu wa Oganaizesheni ni Ndugu Mohamed Seif Khatibu.
  5. Katibu wa Siasa na Mahusiano ya Kimataifa, Asha-rose Migiro.
  6. Katibu wa Uchumi na Fedha, Zakhia A. Meghji.

Baada ya mapendekezo hayo, Halmashauri Kuu ya Taifa ilipitisha majina hayo na kuyakubali kuwa hao waliopendekezwa ndio hasa wanaofaa kuwa wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Pia, Mwenyekiti akawashukuru wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa waliopita na pia kuwataka wajumbe wapya kuchapa kazi, na kuwataka kujenga mustakabali wa Chama, Uimara na Umadhubuti kwa kufanya kazi kwa kushirikiana na kusaidiana.
 
CHANZO: CCM BLOG

KUTOKA MKUTANO MKUU WA CCM TAIFAMakamba azima kura za maruhani


  *Kikwete apeta kwa kushindo

  *Kura zapigwa kufuata mikoa

Wajumbe mbalimbali katika upigaji wa kura
Katika kile kilichoonekana kuepusha jaribio la baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupiga kura ya maruhani dhidi ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete,  Katibu Mkuu Mstaafu, Yusuf Makamba, jana aliuteka Mkutano Mkuu wa Chama hicho kwa kuwapiga vijembe wanachama wanaodaiwa kupanga njama hizo.

Makamba alipewa fursa ya kumnadi Rais  Kikwete kwenye mkutano huo muda mfupi kabla wajumbe kupiga kura za mwenyekiti.

Kabla ya Makamba kumnadi Rais Kikwete, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisoma wasifu wa Kikwete kwa wajumbe wa mkutano huo.

Hatua ya Makamba kushusha vijembe ilifuatia taarifa za uvumi siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano huo wiki iliyopita kuwa  kulikuwa na mpango wa baadhi ya wanachama kutaka kupiga kura za maruhani zenye lengo la kumpunguzia madaraka, Rais Kikwete.

Habari hizo zileleza kuwa kundi moja la wanaotaka urais wa mwaka 2015 kupitia CCM liliandaa mpango wa kumpigia Rais Kikwete kura za hapana kwa lengo la kutaka nafasi ya uenyekiti itengenishwe na urais ili kumpunguzia kazi rais.

Makamba ambaye muda wote wa hotuba yake alikuwa akinukuu vitabu vitakatifu vya Biblia na Koran, aliwaonya wanachama wa chama hicho kuepuka kupiga kura za maruhani zenye lengo la kumpunguzia madaraka Rais Kikwete.

“Umeingia kiongozi, Chama tukiwa na magari aina ya Mahndra tu, lakini leo hii kila mkoa ina Hard top halafu leo mnasema mnataka kupiga kura za maruhani ili mwenyekiti awe nani?” alihoji Makamba.

Alisema wanachama wenye nia ya kupiga kura za maruhani washindwe kwa jina la Yesu na kwamba labda atakayepiga kura ya maruhani atakuwa ni yule tu ambaye amebeba shetani mgongoni.

Hotuba ya Makamba iliwavutia wajumbe wa mkutano huo ambao walishindwa kuvumilia na kuanza kumwendea na kumtunza fedha jukwaani na hivyo kulazimika kusitisha kwa muda kuendelea kuzungumza ili kupata fursa ya kukusanya pesa hizo hali iliyozua vicheko kutoka kwa wajumbe na viongozi waliokuwa meza kuu.

Alisema Rais Kikwete ni mtu wa watu ambaye amekuwa akijitahidi kuhudhuria shughuli kadhaa ikiwamo kwenye mazishi na kutembelea wagonjwa tofauti na viongozi wengine ambao hawafanyi hivyo.

“Kuna wasaidizi wako, mtu akikupigia kura inapokelewa na mkewe anakwambia mzee amelala, lakini wewe (Kikwete) hauko hivyo unapokea simu muda wote hadi saa nane usiku,”alisema Makamba na kuongeza kuwa akiwa Katibu Mkuu wa CCM alipata tabu sana kutokana na kusema ukweli.

“Nasema hivi kwa sababu kuna watu hapa wanasema eti tumpunguzie Mwenyekiti kazi moja kwa kupiga kura za maruhani ili iwe nini?” alihoji na kuongeza:

“Tembo hashindwi kubeba mikonga yake miwili, mlishawahi kumuona ameanguka kwa kubeba mikonga yake.”

Katika kuonyesha kuwapiga vijembe wenye nia hiyo ya kumpunguzia madaraka Kikwete, Makamba alisema huyo anayesema hivyo kazi yake moja tu inamshinda.

Alisema adhabu ya watu wasiokuwa karibu na wananchi imeonekana kwa baadhi ya watu walioshindwa kuchaguliwa kwenye chaguzi ndani ya chama hicho.

Alimsifu Kikwete kwa kuwa kocha mzuri ambaye chama kiliingia mkataba naye toka mwaka mwaka 2005 na 2010.

Makamba alisema safari ya Ikulu inaanzia kwenye mkutano mkuu wa CCM na ili wanachama waende salama ni lazima waende na kocha mzuri.

“Tukisha kuchagua hapa kesho na keshokutwa utakapokwenda kwenye  Kamati Kuu utatafuta kamati ya ufundi tu, lakini kocha ni wewe,” alisema Makamba.

Akinukuu vifungu mbalimbali vya Biblia na Koran, Makamba aliwataka wajumbe wa mkutano huo wasifanye makosa kwa kumuomba Mungu asimame pamoja nao ili awachagulie kiongozi wa CCM.

“Shetani asipite kwenye milango ile, asipenye kwenye kuta hizi, leo mnachagua mtumishi wa Mungu siyo Mwenyekiti wa CCM Taifa tu, Jakaya siyo Malaika ni binadamu ana watoto na wajukuu, hakuna haja ya kumhukumu katika mambo ambayo hayana msingi,” alisema huku akishangiliwa.

Akiendelea kunukuu vitabu hivyo vitakatifu, Makamba alisema Mungu anapenda kuombwa, lakini wapo baadhi ya watu wanamuomba vibaya, kwa manufaa yao binafsi na ndiyo maana hawafanikiwi.

Alisema wajumbe wa mkutano huo wasiangalie dosari za Kikwete kama binadamu.
Makamba katika hotuba yake hiyo aliwageukia watu wanaousaka urais 2015 kwa kueleza kuwa: “Unasema nautaka urais 2015 kumbe anayekufahamu ni mama Janury (mke wake Makamba) tu.”

KURA ZAPIGWA KIMKOA

Kamati ya Uchaguzi ilibadili utaratibu wake wa kupiga kura ambapo jana wajumbe walilazimika kupiga kura kwa kufuata mikoa yao wanayotoka.

Akitangaza kubadilika kwa utaratibu huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, alisema  kila mkoa utakuwa na sanduku lake lililoandikwa mkoa  husika.

“Utaratibu ni kwamba kila mkoa utakuwa na sanduku liloandikwa mkoa wake,” alisema Spika Makinda baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuelezea utaratibu utakaotumika.

Hata hivyo, utaratibu uliotumika kupiga kura ya Mwenyekiti na makamu wake wawili, haukutumika wakati wa kupiga kura za kuwachagua Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).

Aidha, utaratibu huo haujawahi kutokea tangu Chama hicho kilipozaliwa katika mikutano yake saba ya 1977, 1982, 1987, 1992, 1997, 2002 na 2007.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa utaratibu huo ulilenga kufuatilia kwa karibu na kudhibiti mpango wa kupiga kura za maruhani.

Chini ya utaratibu huo kila Katibu wa Mkoa alitakiwa kufika katika meza ya kamati hiyo na kuchukua karatasi za kupigia kura kulingana na idadi ya wajumbe wanaotoka katika mkoa wake.

Kura zilizoanza kupigwa zilikuwa za mwenyekiti na makatibu walitakiwa kuambatana na vijana waliokuwa na sanduku la mikoa yao kukusanya kura.

Wiki iliyopita kabla wajumbe kuwasili mjini Dodoma NIPASHE liliripoti kuwa baadhi ya  wajume wa mkutano mkuu kutoka  mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga kudaiwa  kuhongwa Sh. milioni tatu kila mmoja ili kulikataa jina la Rais  Kikwete.

Alipoulizwa kuhusiana na Mpango huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hata yeye  alizisikia habari hizo, lakini kama lipo jambo hilo si zuri.

MAAZIMIO YA WAJUMBE

Wajumbe wa mkutano huo wamewataka wazee wa Chama hicho na Kamati ya Maadili kuwaita wanachama wanaoleta mgawanyiko ndani ya chama, kuwakemea na wale watakaoendelea na kutumia rushwa kwenye chaguzi waondolewe uanachama.

“Tuvunje makundi yote na wale watakaoonekana kuendeleza makundi Kamati ya Maadili iwaite, kuwaonya na wakikaidi iwafukuze,” alisema msemaji wa kundi la 11, Charles Mwakipesile, ambaye kundi lake lilijumuisha mikoa ya Mbeya, Katavi, Njombe, Mwanza, Kagera, Mara na Morogoro.

Pia, kundi hilo lilipendekeza kiundwe kikosi kazi kitakachovunja makundi ndani ya Chama na kuondoa mmomonyoko.

Katika kuondoa mgawanyiko na mipasuko ndani ya Chama, kundi hilo lilisema kuwa hakuna budi kuepuka watu wanaotumia rushwa kama kigezo cha kupata uongozi.

Mwakipesile alisema wanachama wanaondekeza rushwa kwa kutoau kupokea rushwa ndani ya Chama wanakiletea sifa mbaya Chama na waondolewe.

Kundi hilo lilipendekeza kuwepo watu watakaokuwa wakifanya kazi za propaganda kujibu hoja za uongo zinazotolewa na viongozi wa vyama vya upinzani.

Alidai kuwa wapinzani mara kwa mara wanatoa kauli za uongo dhidi ya CCM na ili kukabiliana nao, ni lazima waimarishe kitengo cha propaganda kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa ili pamoja na mambo mengine, waweze kueleza ukweli wa masuala mbalimbali yanayopotoshwa na viongozi wa vyama ya upinzani.

Alitaka pia ujengwe mkakati wa kuwaingiza kwenye chama ili kujenga CCM imara na yenye nguvu.

“Watani zetu wamekuwa wakiwatumia vijana kwa kuwarubuni, sasa umefika wakati wa kuandaa mkakati wa kujenga vijana,” alisema.

Vile vile, kundi hilo lilipendekeza wanafunzi kuanzia chuo, shule za sekondari wajengewe uwezo wa kuingia kwenye Chama ili itakapofika uchaguzi wa 2015 wawe wapiga kura wa CCM.

Akiwasilisha maoni ya kundi kutoka mikoa ya Dodoma, Iringa, Tanga, Rukwa, Mjini Magharibi, Wilson Mukasa, ambaye ni Katibu wa Tawi la CCM Kizota, alisema wapo wanachama wanaokipaka matope Chama hicho ambao wana ndimi mbili na akataka Kamati ya Maadili ya Chama hicho ihakikishe kwamba inawashughulikia kwa kuwa hawafai kuwa ndani ya chama.

Aidha, kundi hilo lilikishauri Chama hicho kufanya maamuzi sahihi na wakati sahihi, kwani yapo mengine yanayochangia kuwanyima kura wakati wa chaguzi.

Alisema kwa mfano, uamuzi wa kuwahamisha wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni, shughuli kama hii isifanyike wakati wa kuelekea uchauguzi na ikiwezekana iahirishwe hadi wakati mwingine mwafaka kwani zinachangia kuwanyima kura.

Alitaka mawaziri wapewe nafasi kila wiki kwenye televisheni kuelezea shughuli mbalimbali za utekelezaji wa Ilani ya CCM ili wananchi waone na kuelewa kama alivyofanya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, wakati akitoa maelezo ya utekelezaji wa wizara yake mbele ya wajumbe wa mkutano huo juzi.

Katika hatua nyingine, Mukasa aliwataka wajumbe viongozi wa juu wa chama hicho, kuwajali viongozi wa chini wa ngazi ya matawi na mashina, ili Chama hicho kisionekane machoni pa wananchi kuwa ni cha vigogo.

“Viongozi wa chini wanajiona kama wameachwa, na CCM inaonekana kuwa ni ya viongozi wa juu…tunaomba muwawezeshe na kuwapa semina, hali ilivyo sasa hivi inaonekana kuwa chama ni cha vigogo huku wakipita na magari yao wakiwa wamefunga vioo,” alisema.

Aidha, alisema ili kuondoa mgawanyiko na mipazuko ndani ya Chama iwekwe mikakati ya kuepuka rushwa ndani na nje ya chama.

Akizungumzia utaratibu huo wa wajumbe kujadili ilani ya Chama kwenye makundi, alisema umeleta ufanisi mkubwa kwa kupata mawazo mengi ya kukiboresha Chama.

Alisema tofauti na utaratibu wa zamani ambao kila mkoa ulikuwa ukileta taarifa yake, utaratibu huo umeonyesha kuleta ufanisi.

Kuhusu maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe katika kukiimarisha Chama na Serikali, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliomba muda wa miezi miwili au mitatu ili waweze kuyafanyia kazi.

Aliahidi kuwa mapendekezo yote yatawekwa kwenye vijitabu kama taarifa na kusambazwa katika mikoa yote ili wajumbe na wananchi waweze kuyaona.

Kadhalika, Pinda alisema wanafanyia kazi mapendekezo ya utaratibu wa mawaziri kueleza utendaji wao katika sekta mbalimbali wanazofanyia kazi kwenye vyombo vya habari ili wananachi waweze kuona.

Wakati huo huo: Rais Jakaya Kikwete amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Kikwete alichaguliwa kushika wadhifa huo jana na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika katika Ukumbi wa Kizota uliopo nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Akitangaza matokeo hayo jana usiku, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema Kikwete ameibuka mshindi kwa kupata kura 2,395 sawa na asilimia 99.92. Kwa mujibu wa Makinda kura mbili kati ya 2397 ziliharibika.

Alisema Philip Mangula alichaguliwa kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara kwa kuzoa kura zote 2397 sawa na asilimia 100.

Alisema Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kwa kura 2397 sawa na asilimia 100.

Alisema hakuna kura zilizoharibika katika uchaguzi huo.

Awali, akitangaza Spika Makinda alisema wajumbe 20 wa Halmashauri Kuu ya CCM waliochaguliwa juzi kuwa 10 ni kutoka Zanzibar na wengine 10 Tanzania Bara.

Kwa upande wa Zanzibar aliwataja waliochaguliwa kuwa ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa kwa kura 1850, Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif  Khatib (1,668),  Hadija Abdi (1,625), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,  Shamsi Vuai Nahodha (1,603), Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi (1,579), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano),  Samia Hassan Suluhu (1,525), Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Omar Yusuf Mzee 1,415, Bagwaji Mansulia 1,406, Abrakhim Chasama 1,248 na Hamisi Mambo 1,233.

Tanzania Bara ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba (2,093), Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (2,012), Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martin Shigella (1,824), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) (1,805), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (1,455), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo (1,414), Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama (1,374), Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Jackison Msome (1,202), Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara (984).

Akizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa, Katibu wa Halamshauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Mnauye alitamba kwa kusema kuwa wamepeleka kilio upinzani huku akisisitiza walidhani CCM watashindwa katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Kikwete aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kumchagua kuwa mwenyekiti tena wa chama hicho.

Imeandikwa na Beatrice Bandawe, John Ngunge, Sharon Sauwa, Dodoma na Thobias Mwanakatwe, Dar.
CHANZO: NIPASHE

WANA CCM DIASPORA WATIA FORA KIZOTA, DODOMA

WANA CCM DIASPORA WATIA FORA KIZOTA, DODOMA

 Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wa juu wa CCM katika picha ya pamoja na viongozi wa matawi ya CCM ughaibuni (mkoa wa Diaspora) wakiwa katika mkutano Mkuu wa nane wa chama hicho huko Kizota mjini Dodoma leo
 Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakisalimiana na  viongozi wa matawi ya CCM ughaibuni (mkoa wa Diaspora) wakiwa katika mkutano Mkuu wa nane wa chama hicho huko Kizota mjini Dodoma leo
 Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Katibu wa CCM tawi la Diaspora UK  Mariamu Mungula
 Waziri Mkuu Mizengo Pinda akipozi na  viongozi wa matawi ya CCM ughaibuni (mkoa wa Diaspora) wakiwa katika mkutano Mkuu wa nane wa chama hicho huko Kizota mjini Dodoma leo

Viongozi wa matawi ya CCM ughaibuni (mkoa wa Diaspora) wakiwa katika mkutano Mkuu wa nane wa chama hicho huko Kizota mjini Dodoma jana. PICHA NA IKULU

Tuesday, November 6, 2012

Pigo kubwa Chadema Madiwani, Mkurugenzi, Makatibu Wakutwa na hatia


 
Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Mwanza imewatia hatiani viongozi watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwamo madiwani wawili kwa kosa la kukaidi amri ya Mahakama.
Viongozi waliotiwa hatiani ni madiwani Dan Kahungu wa Kata ya Kirumba na Josephat Manyerere wa Kata ya Nyakato ambaye kabla ya kuondolewa kwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye alikuwa ndiye Meya wa Jiji la Mwanza.
Viongozi wengine wa Chadema waliotiwa hatiani na Mahakama hiyo ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema Taifa, Benson Kigaila, Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, John Anajus na Katibu Mwenezi wa wilaya hiyo, Carlos Majura.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Angelo Rumisha, ndiye aliyewatia hatiani viongozi hao, lakini hakutamka adhabu watakayotumikia kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kutokana na baadhi ya watuhumiwa kutokuwepo mahakamani hapo.
Diwani Kahungu na Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Anajus ndio waliokuwepo mahakamani wakati Hakimu Rumisha akitangaza kuwatia hatiani na aliamuru wapelekwe rumande hadi wenzao watatu watakapokamatwa na kufikishwa mahakamani.

Mbali na kuwatia hatiani viongozi hao wa Chadema, Hakimu Rumisha alisema kwamba maamuzi ya awali yaliyotolewa na Mahakama ya kutengua hatua ya Matata na mwenzake kuvuliwa uanachama yatabaki kama yalivyo hadi itakapoamuliwa vinginevyo katika kesi ya msingi.
Hatua hiyo ya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi jijini Mwanza kuwatia hatiani viongozi hao wa Chadema, inafuatia tukio la Kamati Kuu ya Chadema kuwavua uanachama madiwani Henry Matata wa Kata ya Kitangiri na Adam Chagulani wa Kata ya Igoma.
Baada ya madiwani hao kuvuliwa uanachana, Matata alifungua kesi ya kupinga hatua hiyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi jijini Mwanza ilitoa amri ya kutaka madiwani hao wasizuiwe kuendelea na shughuli zao na watambuliwe kama wanachama halali wa Chadema
Hata hivyo, Septemba 25, mwaka huu, Chadema Wilaya ya Ilemela kilifanya mkutano wa uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Meya na Naibu Meya wa manispaa hiyo, hatua ambayo inaonekana kuwa sababu ya Diwani Matata kuamua kufungua kesi dhidi ya baadhi ya washiriki wa mkutano huo akiwamo Kigaila (Mkurugenzi wa Oganaizesheni) akiwatuhumu kukiuka amri ya Mahakama kwa kutomshirikisha.
Oktoba 13 mwaka huu baadhi ya magazeti yalichapisha habari kuhusiana na malalamiko ya Chadema Wilaya ya Ilemela kwamba zipo njama zinazomhusisha Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Angelo Rumisha, za kutaka kukihujumu chama hicho katika uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela.
Chama hicho kilidai kwamba hujuma hiyo inalenga kutaka kuwahukumu kifungo cha miezi sita jela madiwani wake wawili ili wasipate fursa ya kushiriki uchaguzi wa Meya na Naibu wake unaotarajiwa kufanyika hapo baadaye baada ya kuahirishwa katika mazingira ya kutatanisha.
Kufuatia kuwepo kwa tetesi hizo, Chadema kiliamua kumuandikia barua Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kumtaka aingilie kati suala hilo na kuhakikisha haki inatendeka.
Katika barua hiyo yenye Kumbukumbu Namba CDM/w.IL/2012/01 ya tarehe 11/10/2012 ambayo ilisainiwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Yunus Chilongozi, kwenda kwa Jaji Mfawidhi, chama hicho kilidai kwamba Madiwani wanaolengwa katika mpango huo ni Dan Kahungu wa Kata ya Kirumba na Josephat Manyerere wa Kata ya Nyakato.
Mbali na madiwani hao, barua hiyo iliwataja watu wengine wanaolengwa katika njama hizo kuwa ni Kigaila, Anajus, Majura na Baraza la Wadhamini la chama hicho.
Chadema kimedai katika barua yake hiyo kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Mwanza imeamua kukubali maombi yenye lengo la kutaka kuwatia hatiani viongozi hao kama wafungwa wa kimadai (civil prisoners) kwa kosa la kutotii amri ya Mahakama.
“Mheshimiwa jaji Mfawidhi, maombi hayo yaliyowasilishwa na Henry Mtinda Matata kupitia mawakili wake, Magongo na Matata, yakasajiliwa kama Misc.
Application No.66/2012 yanaonekana yamelenga hasa madiwani hao wawili kama njia ya kuwakomoa na kuwasababishia kukosa nafasi ya kushiriki uchaguzi wa umeya wa Manispaa mpya ya Ilemela,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Blogger