Posted by MENACO on 12:18:00 PM
Nakusudia kutumia kifungu cha 10 cha Sheria
ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa
mkopo wa masharti kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi
trilioni 1.86) kutoka China.
Nitataka pia nakala za mikataba
wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa
mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na
ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka
Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa
532.
Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini
haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012
kwamba kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha
ya wananchi wa sasa na baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na
kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika.
Pendekezo hilo
lingeliwezesha Bunge kuishauri na kuisimamia serikali kuanzia katika
hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa yanalindwa katika
hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji
huo mkubwa.
Kutokana na Serikali kutokuzingatia pendekezo hilo
na badala yake Rais Jakaya Kikwete kufanya uzinduzi wa mradi huo tarehe
8 Novemba 2012 Mkoani Dar es salaam huku usiri ukiendelezwa malalamiko
yameanza kujitokeza katika maeneo ya mradi husika hususan katika Mkoa wa
Mtwara.
Aidha, Serikali irejee katika mapendekezo niliyotoa
bungeni na kutoa maelezo kwa umma ya sababu za bomba hilo kujengwa
kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam na kueleza kwa uwazi manufaa ya mradi
huo na miradi mingine inayopaswa kutekelezwa katika mikoa ya Kusini kwa
maendeleo ya wananchi husika.
Tarehe 27 Julai 2012 nilieleza
bungeni kuwa pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi
asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo; Serikali
inapaswa kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo ambayo
imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo
kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na
MW 230 wa Somanga Fungu (Kilwa).
Kwa upande mwingine,
utekelezaji wa mradi huo unaendelea bila kuwa na Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini ambayo ingepaswa kuishauri na kuisimamia
Serikali hivyo ni muhimu Spika wa Bunge akachukua hatua kutokana na
barua niliyomwandikia mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2012 ambayo mpaka sasa
haijajibiwa.
Ikumbukwe kwamba katika barua hiyo nilitoa mwito
kwa Spika atumie madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati
nyingine ya kudumu ya Bunge itayoshughulikia nishati na madini ikiwemo
masuala ya gesi asili kwa sasa kufuatia hali tete na tata kuhusu sekta
ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta
hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Pamoja na
mambo mengine nilipendekeza Spika aelekeze kamati hiyo kupokea na
kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011
kuhusu Sekta Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika
kushughulikia tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha za mauzo ya
Gesi asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango
mkakati na sheria ya gesi asili.
Hatua hii ni muhimu kwa sasa
kwa kuwa hata baada ya uamuzi wake kuhusu tuhuma za rushwa kwa wajumbe
wa Kamati husika, Spika hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini
iliyovunjwa hali ambayo imeacha ombwe la uongozi na usimamizi wa kibunge
(Parliamentary Oversight) kwenye sekta hizi nyeti kwa uchumi wa nchi na
maisha ya wananchi.
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
0 comments:
Post a Comment