Unordered List

Pages

Monday, October 29, 2012

Uchaguzi wa madiwani vurugu tupu

*Mkoani Arusha risasi za moto zarindima mchana kweupe
*Songea, wafuasi wa CCM, CHADEMA wakatana mapanga
*Chadema yashinda Ludewa, CCM yashinda Songea
MBUNGE wa Viti Maalum, Rahel Mashishanga (CHADEMA) pamoja na Katibu wa Chadema Jimbo la Nyang’hwale mkoani Geita, Michael Ndege, wamenusurika kuuawa baada ya kuvamiwa na kisha kupigwa na kukatwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Viongozi hao walivamiwa jana katika matukio tofauti, ambapo Mashishanga anadaiwa kuvamiwa jana asubuhi, alipokuwa akiangalia mwenendo wa uchaguzi wa udiwani katika vituo vya kupigia kura, katika Kata ya Mwawaza, mkoani Shinyanga.

Akiwa katika kazi hiyo, inasemekana mbunge huyo alivamiwa na kundi la vijana, wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.

Akizungumza na MTANZANIA jana kwa simu kutoka mkoani Shinyanga, Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), alisema Mashishanga alivamiwa na kupigwa na gari lake liliharibiwa vibaya, kwa kupigwa mawe.

“Ni kweli nimeambiwa Mbunge Rahel Mashishanga, amevamiwa na kupigwa na wafuasi wa CCM, wakati akitembelea na kuona zoezi la upigaji kura katika Kata ya Mwawaza.

“Mbali na kumpiga, wameiponda kwa mawe gari yake na vioo vinaelezwa vimeharibika vyote. Mbaya zaidi alikuwa na mdogo wake, ambaye amepigwa na kuteguka bega la kushoto na ameumia mdomo.

“Kwa sasa mimi nipo hapa kama mwangalizi wa uchaguzi, ambaye ninakisimamia chama changu katika uchaguzi wa Kata hii ya Mwawaza,” alisema Nyerere.

Vincent ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema kuwa vitendo hivyo kamwe havivumiliki, huku akilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linawasaka na kuwakamata watu wote waliohusika katika tukio hilo.

Kwa upande wake, Ndege inasemekana alivamiwa juzi usiku akiwa njiani kwenda kulala, ambapo alivamiwa na kundi la vijana waliokuwa wamevalia sare za CCM, kisha akakatwa kwa mapanga na visu.

MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala, ili kuthibitisha kutokea kwa matukio hayo, alisema hana taarifa ingawa aliahidi kufuatilia.

SOURCE: MTANZANIA (GAZETI)

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Blogger