Unordered List

Pages

Wednesday, November 14, 2012

KUTOKA MKUTANO MKUU WA CCM TAIFAMakamba azima kura za maruhani


  *Kikwete apeta kwa kushindo

  *Kura zapigwa kufuata mikoa

Wajumbe mbalimbali katika upigaji wa kura
Katika kile kilichoonekana kuepusha jaribio la baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupiga kura ya maruhani dhidi ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete,  Katibu Mkuu Mstaafu, Yusuf Makamba, jana aliuteka Mkutano Mkuu wa Chama hicho kwa kuwapiga vijembe wanachama wanaodaiwa kupanga njama hizo.

Makamba alipewa fursa ya kumnadi Rais  Kikwete kwenye mkutano huo muda mfupi kabla wajumbe kupiga kura za mwenyekiti.

Kabla ya Makamba kumnadi Rais Kikwete, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisoma wasifu wa Kikwete kwa wajumbe wa mkutano huo.

Hatua ya Makamba kushusha vijembe ilifuatia taarifa za uvumi siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano huo wiki iliyopita kuwa  kulikuwa na mpango wa baadhi ya wanachama kutaka kupiga kura za maruhani zenye lengo la kumpunguzia madaraka, Rais Kikwete.

Habari hizo zileleza kuwa kundi moja la wanaotaka urais wa mwaka 2015 kupitia CCM liliandaa mpango wa kumpigia Rais Kikwete kura za hapana kwa lengo la kutaka nafasi ya uenyekiti itengenishwe na urais ili kumpunguzia kazi rais.

Makamba ambaye muda wote wa hotuba yake alikuwa akinukuu vitabu vitakatifu vya Biblia na Koran, aliwaonya wanachama wa chama hicho kuepuka kupiga kura za maruhani zenye lengo la kumpunguzia madaraka Rais Kikwete.

“Umeingia kiongozi, Chama tukiwa na magari aina ya Mahndra tu, lakini leo hii kila mkoa ina Hard top halafu leo mnasema mnataka kupiga kura za maruhani ili mwenyekiti awe nani?” alihoji Makamba.

Alisema wanachama wenye nia ya kupiga kura za maruhani washindwe kwa jina la Yesu na kwamba labda atakayepiga kura ya maruhani atakuwa ni yule tu ambaye amebeba shetani mgongoni.

Hotuba ya Makamba iliwavutia wajumbe wa mkutano huo ambao walishindwa kuvumilia na kuanza kumwendea na kumtunza fedha jukwaani na hivyo kulazimika kusitisha kwa muda kuendelea kuzungumza ili kupata fursa ya kukusanya pesa hizo hali iliyozua vicheko kutoka kwa wajumbe na viongozi waliokuwa meza kuu.

Alisema Rais Kikwete ni mtu wa watu ambaye amekuwa akijitahidi kuhudhuria shughuli kadhaa ikiwamo kwenye mazishi na kutembelea wagonjwa tofauti na viongozi wengine ambao hawafanyi hivyo.

“Kuna wasaidizi wako, mtu akikupigia kura inapokelewa na mkewe anakwambia mzee amelala, lakini wewe (Kikwete) hauko hivyo unapokea simu muda wote hadi saa nane usiku,”alisema Makamba na kuongeza kuwa akiwa Katibu Mkuu wa CCM alipata tabu sana kutokana na kusema ukweli.

“Nasema hivi kwa sababu kuna watu hapa wanasema eti tumpunguzie Mwenyekiti kazi moja kwa kupiga kura za maruhani ili iwe nini?” alihoji na kuongeza:

“Tembo hashindwi kubeba mikonga yake miwili, mlishawahi kumuona ameanguka kwa kubeba mikonga yake.”

Katika kuonyesha kuwapiga vijembe wenye nia hiyo ya kumpunguzia madaraka Kikwete, Makamba alisema huyo anayesema hivyo kazi yake moja tu inamshinda.

Alisema adhabu ya watu wasiokuwa karibu na wananchi imeonekana kwa baadhi ya watu walioshindwa kuchaguliwa kwenye chaguzi ndani ya chama hicho.

Alimsifu Kikwete kwa kuwa kocha mzuri ambaye chama kiliingia mkataba naye toka mwaka mwaka 2005 na 2010.

Makamba alisema safari ya Ikulu inaanzia kwenye mkutano mkuu wa CCM na ili wanachama waende salama ni lazima waende na kocha mzuri.

“Tukisha kuchagua hapa kesho na keshokutwa utakapokwenda kwenye  Kamati Kuu utatafuta kamati ya ufundi tu, lakini kocha ni wewe,” alisema Makamba.

Akinukuu vifungu mbalimbali vya Biblia na Koran, Makamba aliwataka wajumbe wa mkutano huo wasifanye makosa kwa kumuomba Mungu asimame pamoja nao ili awachagulie kiongozi wa CCM.

“Shetani asipite kwenye milango ile, asipenye kwenye kuta hizi, leo mnachagua mtumishi wa Mungu siyo Mwenyekiti wa CCM Taifa tu, Jakaya siyo Malaika ni binadamu ana watoto na wajukuu, hakuna haja ya kumhukumu katika mambo ambayo hayana msingi,” alisema huku akishangiliwa.

Akiendelea kunukuu vitabu hivyo vitakatifu, Makamba alisema Mungu anapenda kuombwa, lakini wapo baadhi ya watu wanamuomba vibaya, kwa manufaa yao binafsi na ndiyo maana hawafanikiwi.

Alisema wajumbe wa mkutano huo wasiangalie dosari za Kikwete kama binadamu.
Makamba katika hotuba yake hiyo aliwageukia watu wanaousaka urais 2015 kwa kueleza kuwa: “Unasema nautaka urais 2015 kumbe anayekufahamu ni mama Janury (mke wake Makamba) tu.”

KURA ZAPIGWA KIMKOA

Kamati ya Uchaguzi ilibadili utaratibu wake wa kupiga kura ambapo jana wajumbe walilazimika kupiga kura kwa kufuata mikoa yao wanayotoka.

Akitangaza kubadilika kwa utaratibu huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, alisema  kila mkoa utakuwa na sanduku lake lililoandikwa mkoa  husika.

“Utaratibu ni kwamba kila mkoa utakuwa na sanduku liloandikwa mkoa wake,” alisema Spika Makinda baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuelezea utaratibu utakaotumika.

Hata hivyo, utaratibu uliotumika kupiga kura ya Mwenyekiti na makamu wake wawili, haukutumika wakati wa kupiga kura za kuwachagua Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).

Aidha, utaratibu huo haujawahi kutokea tangu Chama hicho kilipozaliwa katika mikutano yake saba ya 1977, 1982, 1987, 1992, 1997, 2002 na 2007.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa utaratibu huo ulilenga kufuatilia kwa karibu na kudhibiti mpango wa kupiga kura za maruhani.

Chini ya utaratibu huo kila Katibu wa Mkoa alitakiwa kufika katika meza ya kamati hiyo na kuchukua karatasi za kupigia kura kulingana na idadi ya wajumbe wanaotoka katika mkoa wake.

Kura zilizoanza kupigwa zilikuwa za mwenyekiti na makatibu walitakiwa kuambatana na vijana waliokuwa na sanduku la mikoa yao kukusanya kura.

Wiki iliyopita kabla wajumbe kuwasili mjini Dodoma NIPASHE liliripoti kuwa baadhi ya  wajume wa mkutano mkuu kutoka  mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga kudaiwa  kuhongwa Sh. milioni tatu kila mmoja ili kulikataa jina la Rais  Kikwete.

Alipoulizwa kuhusiana na Mpango huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hata yeye  alizisikia habari hizo, lakini kama lipo jambo hilo si zuri.

MAAZIMIO YA WAJUMBE

Wajumbe wa mkutano huo wamewataka wazee wa Chama hicho na Kamati ya Maadili kuwaita wanachama wanaoleta mgawanyiko ndani ya chama, kuwakemea na wale watakaoendelea na kutumia rushwa kwenye chaguzi waondolewe uanachama.

“Tuvunje makundi yote na wale watakaoonekana kuendeleza makundi Kamati ya Maadili iwaite, kuwaonya na wakikaidi iwafukuze,” alisema msemaji wa kundi la 11, Charles Mwakipesile, ambaye kundi lake lilijumuisha mikoa ya Mbeya, Katavi, Njombe, Mwanza, Kagera, Mara na Morogoro.

Pia, kundi hilo lilipendekeza kiundwe kikosi kazi kitakachovunja makundi ndani ya Chama na kuondoa mmomonyoko.

Katika kuondoa mgawanyiko na mipasuko ndani ya Chama, kundi hilo lilisema kuwa hakuna budi kuepuka watu wanaotumia rushwa kama kigezo cha kupata uongozi.

Mwakipesile alisema wanachama wanaondekeza rushwa kwa kutoau kupokea rushwa ndani ya Chama wanakiletea sifa mbaya Chama na waondolewe.

Kundi hilo lilipendekeza kuwepo watu watakaokuwa wakifanya kazi za propaganda kujibu hoja za uongo zinazotolewa na viongozi wa vyama vya upinzani.

Alidai kuwa wapinzani mara kwa mara wanatoa kauli za uongo dhidi ya CCM na ili kukabiliana nao, ni lazima waimarishe kitengo cha propaganda kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa ili pamoja na mambo mengine, waweze kueleza ukweli wa masuala mbalimbali yanayopotoshwa na viongozi wa vyama ya upinzani.

Alitaka pia ujengwe mkakati wa kuwaingiza kwenye chama ili kujenga CCM imara na yenye nguvu.

“Watani zetu wamekuwa wakiwatumia vijana kwa kuwarubuni, sasa umefika wakati wa kuandaa mkakati wa kujenga vijana,” alisema.

Vile vile, kundi hilo lilipendekeza wanafunzi kuanzia chuo, shule za sekondari wajengewe uwezo wa kuingia kwenye Chama ili itakapofika uchaguzi wa 2015 wawe wapiga kura wa CCM.

Akiwasilisha maoni ya kundi kutoka mikoa ya Dodoma, Iringa, Tanga, Rukwa, Mjini Magharibi, Wilson Mukasa, ambaye ni Katibu wa Tawi la CCM Kizota, alisema wapo wanachama wanaokipaka matope Chama hicho ambao wana ndimi mbili na akataka Kamati ya Maadili ya Chama hicho ihakikishe kwamba inawashughulikia kwa kuwa hawafai kuwa ndani ya chama.

Aidha, kundi hilo lilikishauri Chama hicho kufanya maamuzi sahihi na wakati sahihi, kwani yapo mengine yanayochangia kuwanyima kura wakati wa chaguzi.

Alisema kwa mfano, uamuzi wa kuwahamisha wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni, shughuli kama hii isifanyike wakati wa kuelekea uchauguzi na ikiwezekana iahirishwe hadi wakati mwingine mwafaka kwani zinachangia kuwanyima kura.

Alitaka mawaziri wapewe nafasi kila wiki kwenye televisheni kuelezea shughuli mbalimbali za utekelezaji wa Ilani ya CCM ili wananchi waone na kuelewa kama alivyofanya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, wakati akitoa maelezo ya utekelezaji wa wizara yake mbele ya wajumbe wa mkutano huo juzi.

Katika hatua nyingine, Mukasa aliwataka wajumbe viongozi wa juu wa chama hicho, kuwajali viongozi wa chini wa ngazi ya matawi na mashina, ili Chama hicho kisionekane machoni pa wananchi kuwa ni cha vigogo.

“Viongozi wa chini wanajiona kama wameachwa, na CCM inaonekana kuwa ni ya viongozi wa juu…tunaomba muwawezeshe na kuwapa semina, hali ilivyo sasa hivi inaonekana kuwa chama ni cha vigogo huku wakipita na magari yao wakiwa wamefunga vioo,” alisema.

Aidha, alisema ili kuondoa mgawanyiko na mipazuko ndani ya Chama iwekwe mikakati ya kuepuka rushwa ndani na nje ya chama.

Akizungumzia utaratibu huo wa wajumbe kujadili ilani ya Chama kwenye makundi, alisema umeleta ufanisi mkubwa kwa kupata mawazo mengi ya kukiboresha Chama.

Alisema tofauti na utaratibu wa zamani ambao kila mkoa ulikuwa ukileta taarifa yake, utaratibu huo umeonyesha kuleta ufanisi.

Kuhusu maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe katika kukiimarisha Chama na Serikali, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliomba muda wa miezi miwili au mitatu ili waweze kuyafanyia kazi.

Aliahidi kuwa mapendekezo yote yatawekwa kwenye vijitabu kama taarifa na kusambazwa katika mikoa yote ili wajumbe na wananchi waweze kuyaona.

Kadhalika, Pinda alisema wanafanyia kazi mapendekezo ya utaratibu wa mawaziri kueleza utendaji wao katika sekta mbalimbali wanazofanyia kazi kwenye vyombo vya habari ili wananachi waweze kuona.

Wakati huo huo: Rais Jakaya Kikwete amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Kikwete alichaguliwa kushika wadhifa huo jana na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika katika Ukumbi wa Kizota uliopo nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Akitangaza matokeo hayo jana usiku, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema Kikwete ameibuka mshindi kwa kupata kura 2,395 sawa na asilimia 99.92. Kwa mujibu wa Makinda kura mbili kati ya 2397 ziliharibika.

Alisema Philip Mangula alichaguliwa kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara kwa kuzoa kura zote 2397 sawa na asilimia 100.

Alisema Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kwa kura 2397 sawa na asilimia 100.

Alisema hakuna kura zilizoharibika katika uchaguzi huo.

Awali, akitangaza Spika Makinda alisema wajumbe 20 wa Halmashauri Kuu ya CCM waliochaguliwa juzi kuwa 10 ni kutoka Zanzibar na wengine 10 Tanzania Bara.

Kwa upande wa Zanzibar aliwataja waliochaguliwa kuwa ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa kwa kura 1850, Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif  Khatib (1,668),  Hadija Abdi (1,625), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,  Shamsi Vuai Nahodha (1,603), Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi (1,579), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano),  Samia Hassan Suluhu (1,525), Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Omar Yusuf Mzee 1,415, Bagwaji Mansulia 1,406, Abrakhim Chasama 1,248 na Hamisi Mambo 1,233.

Tanzania Bara ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba (2,093), Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (2,012), Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martin Shigella (1,824), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) (1,805), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (1,455), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo (1,414), Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama (1,374), Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Jackison Msome (1,202), Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara (984).

Akizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa, Katibu wa Halamshauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Mnauye alitamba kwa kusema kuwa wamepeleka kilio upinzani huku akisisitiza walidhani CCM watashindwa katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Kikwete aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kumchagua kuwa mwenyekiti tena wa chama hicho.

Imeandikwa na Beatrice Bandawe, John Ngunge, Sharon Sauwa, Dodoma na Thobias Mwanakatwe, Dar.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Blogger