Haina ubishi kuwa J. Kikwete ni rais pekee ametawala kwa mizengwe lakini namna anavyoipangua mizengwe hiyo, anastahili pongezi kubwa. Ikumbukwe zengwe la kwanza ni lile la kukataliwa na CHADEMA kuwa si rais halali, wakaenda mbali zaidi kwa wabunge wake kumzilia hotuba yake ya ufunguzi na kutoka nje ili kumdhalilisha, huku katibu mkuu kutangaza kuwa atahakikisha J.K hatawali.
Kikwete kwa umahiri mkubwa alitulia na kuendelea kuhutubia huku akiwahakikishia kuwa "ipo siku watarudi kwake" (walirudi hawakurudi?). Zengwe lingine ni la kudai kumshtaki J.K kwa wananchi ili kumshinikiza aondoke madarakani. Hili pia lilifanywa na CHADEMA kupitia maandamano sehemu mbalimbali za nchi wakilenga zaidi kutengeneza propaganda ya kuidanganya jumuiya ya kimataifa kuwa J.K hakubaliki na wananchi.
Hilo lilishindwa kwakuwa J.K alitulia na wala hakutaka kutumia nguvu ya dola ambao kimsingi ndiyo mtego ulikuwa umewekwa na CHADEMA. Maandamano yaliposhindwa, ukaanza ushawishi wa migomo kwa wafanyakazi walimu na madaktari, nalo lilishughulikiwa kwa umakini kila mtu anajua. Propaganda ya Ulimboka iliyoshikiwa bango na CHADEMA na wanaharakati kwa kumlazimisha Ulimboka aseme hata yasiyokuwepo, iligonga mwamba.
Zengwe zimezidi kuendelea kupitia M4C ya CHADEMA ambayo kwa mgongo wa elimu ya uraia ililenga kushawishi wananchi kuikataa serikali ya J.K kwa mtindo wa Libya, Tunisia na Misri, hiyo nayo nia wazi wananchi wameishtukia kuwa haina nia nzuri na hatma ya Amani ya Tanzania. Imekataliwa na ushahidi ni matokeo ya udiwani wa kata 29 uliofanyika hivi majuzi ambapo CHADEMA pamoja na nguvu kubwa ya M4C iliambulia kata 5! huku CCM ikijikombea kata 22 kati ya 29 zilizokuwa zinagombewa.
J.K amezidi kuimarisha CCM huku CHADEMA wakichelewa kugombania nani agombee urais/uenyekiti wa chama na kibaya zaidi na bila kujijua wote wamejikuta wanaimba wimbo wa CCM na kukiacha chama kikizidi kuangamia. Aliyozuiliwa Zitto kuyafanya, ndiyo yafanywayo na Mbowe.
Juzi juzi hivi Mbowe amesikika akiupongeza urais wa J.K na kukiri kuwa ni urais uliotukuka uliojaa busara na hekima na kwamba kwa TZ hakuna kama J.K. Kimsingi Slaa amejikuta akibaki peke yake aking'ang'ana na siasa za chuki na utovu wa nidhamu kwa J.K huku wenzake wote waliomzunguka wakimuasi bila yeye kujijua. J.K hajateteleka kiutendaji , zaidi ameendelea kukomaa na kujawa na maarifa zaidi.
Sote tumeshuhudia jinsi serikali ya awamu ya nne ilivyovunja rekodi kwa ujenzi wa miundo kupitia hotuba ya Magufuli wakati wa Mkutano mkuu wa CCM Dodoma.
Kwa hakika J.K ni rais ambaye amewabaini wabaya wake mapema na sasa anacheza nao kama atakavyo. Anajua pia wabaya hao bado wanamtafuta kwani bado hawajakidhi haja ya kiu yao ya kuona J.K akitolewa ikulu kwa madai ya kuushindwa Urais. J.K kweli ni zaidi ya "jembe".
SOURCE: JF
0 comments:
Post a Comment