Mahakama
ya Hakimu Mkazi jijini Mwanza imewatia hatiani viongozi watano wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwamo madiwani wawili kwa kosa
la kukaidi amri ya Mahakama.
Viongozi
waliotiwa hatiani ni madiwani Dan Kahungu wa Kata ya Kirumba na Josephat
Manyerere wa Kata ya Nyakato ambaye kabla ya kuondolewa kwa kupigiwa
kura ya kutokuwa na imani naye alikuwa ndiye Meya wa Jiji la Mwanza.
Viongozi
wengine wa Chadema waliotiwa hatiani na Mahakama hiyo ni Mkurugenzi wa
Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema Taifa, Benson Kigaila, Katibu wa
Chadema Wilaya ya Ilemela, John Anajus na Katibu Mwenezi wa wilaya hiyo,
Carlos Majura.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Angelo Rumisha, ndiye aliyewatia
hatiani viongozi hao, lakini hakutamka adhabu watakayotumikia kwa kile
kilichoelezwa kwamba ni kutokana na baadhi ya watuhumiwa kutokuwepo
mahakamani hapo.
Diwani
Kahungu na Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Anajus ndio waliokuwepo
mahakamani wakati Hakimu Rumisha akitangaza kuwatia hatiani na aliamuru
wapelekwe rumande hadi wenzao watatu watakapokamatwa na kufikishwa
mahakamani.
Mbali na
kuwatia hatiani viongozi hao wa Chadema, Hakimu Rumisha alisema kwamba
maamuzi ya awali yaliyotolewa na Mahakama ya kutengua hatua ya Matata na
mwenzake kuvuliwa uanachama yatabaki kama yalivyo hadi itakapoamuliwa
vinginevyo katika kesi ya msingi.
Hatua
hiyo ya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi jijini Mwanza kuwatia hatiani
viongozi hao wa Chadema, inafuatia tukio la Kamati Kuu ya Chadema
kuwavua uanachama madiwani Henry Matata wa Kata ya Kitangiri na Adam
Chagulani wa Kata ya Igoma.
Baada ya
madiwani hao kuvuliwa uanachana, Matata alifungua kesi ya kupinga hatua
hiyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi jijini Mwanza ilitoa amri ya
kutaka madiwani hao wasizuiwe kuendelea na shughuli zao na watambuliwe
kama wanachama halali wa Chadema
Hata
hivyo, Septemba 25, mwaka huu, Chadema Wilaya ya Ilemela kilifanya
mkutano wa uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Meya na Naibu Meya wa
manispaa hiyo, hatua ambayo inaonekana kuwa sababu ya Diwani Matata
kuamua kufungua kesi dhidi ya baadhi ya washiriki wa mkutano huo akiwamo
Kigaila (Mkurugenzi wa Oganaizesheni) akiwatuhumu kukiuka amri ya
Mahakama kwa kutomshirikisha.
Oktoba 13
mwaka huu baadhi ya magazeti yalichapisha habari kuhusiana na
malalamiko ya Chadema Wilaya ya Ilemela kwamba zipo njama zinazomhusisha
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Angelo Rumisha, za kutaka
kukihujumu chama hicho katika uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Manispaa
ya Ilemela.
Chama
hicho kilidai kwamba hujuma hiyo inalenga kutaka kuwahukumu kifungo cha
miezi sita jela madiwani wake wawili ili wasipate fursa ya kushiriki
uchaguzi wa Meya na Naibu wake unaotarajiwa kufanyika hapo baadaye baada
ya kuahirishwa katika mazingira ya kutatanisha.
Kufuatia
kuwepo kwa tetesi hizo, Chadema kiliamua kumuandikia barua Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kumtaka aingilie kati suala hilo na
kuhakikisha haki inatendeka.
Katika
barua hiyo yenye Kumbukumbu Namba CDM/w.IL/2012/01 ya tarehe 11/10/2012
ambayo ilisainiwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Yunus
Chilongozi, kwenda kwa Jaji Mfawidhi, chama hicho kilidai kwamba
Madiwani wanaolengwa katika mpango huo ni Dan Kahungu wa Kata ya Kirumba
na Josephat Manyerere wa Kata ya Nyakato.
Mbali na
madiwani hao, barua hiyo iliwataja watu wengine wanaolengwa katika njama
hizo kuwa ni Kigaila, Anajus, Majura na Baraza la Wadhamini la chama
hicho.
Chadema
kimedai katika barua yake hiyo kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini
Mwanza imeamua kukubali maombi yenye lengo la kutaka kuwatia hatiani
viongozi hao kama wafungwa wa kimadai (civil prisoners) kwa kosa la
kutotii amri ya Mahakama.
“Mheshimiwa
jaji Mfawidhi, maombi hayo yaliyowasilishwa na Henry Mtinda Matata
kupitia mawakili wake, Magongo na Matata, yakasajiliwa kama Misc.
Application
No.66/2012 yanaonekana yamelenga hasa madiwani hao wawili kama njia ya
kuwakomoa na kuwasababishia kukosa nafasi ya kushiriki uchaguzi wa umeya
wa Manispaa mpya ya Ilemela,” inasema sehemu ya barua hiyo.
0 comments:
Post a Comment