MHOJAJI: Mkuu Zitto nashukuru kwa majibu yako kina kwa swali la kwanza, swali linalofuata;
B. Zitto na CHADEMA
1) Nini kipaumbele chako cha sasa kama mwanachama wa CHADEMA?
2) Mkuu, ni kweli kuwa CHADEMA ni chama cha kidini/kikabila?
Na kama ni kweli, tatizo hilo lishughulikiwe vipi? Kama si kweli,
unaweza kuueleza umma wa watanzania una kauli gani juu ya mitizamo hii
dhidi ya chama chenu?
3) Mh. Zitto, unaizungumziaje demokrasia ndani ya chama chako katika chaguzi, teuzi na kupanga safu za uongozi?
4) Kwanini CHADEMA haiwatumii viongozi wa Mikoa na Wilaya na
badala yake inatuma watu toka makao makuu hata kwa mambo madogo madogo
ambayo yangemalizwa na uongozi wa ngazi husika?
5) Mh Zitto, unazizungumziaje harakati za M4C na athari
(impact) yake kisiasa na kijamii? Chama kimeweka taratibu gani nzuri za
malezi kwa wanachama wapya wanaojiunga kwenye M4C, kama bado, huku si
kusuka kamba inayoungua?
6) Inadaiwa hushiriki kikamilifu M4C, ni kweli? Nini kauli yako dhidi ya tuhuma hizi?
7) Je, utaratibu wa kupita mikoani katika kutafuta nafasi ya
kugombea uenyekiti kama ilivyokuwa wakati wa Mbowe unafaa au CHADEMA
irudi katika utaratibu kama wa CCM?
8) Mhe. Zitto, Viongozi/CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kufichua
ufisadi. Kuna taarifa kuwa kuna mwanachama wenu katafuna fedha za M4C,
ni kweli? Kama ni kweli, ameshughulikiwaje? Kama hajashughulikiwa, ni
kwanini mko kimya?
9) Zitto wewe ni naibu katibu mkuu wa CHADEMA, Mara nyingi
matamko ya chama yametolewa na Katibu, Mwenyekiti, Mnyika (tangu kabla
hajawa msemaji) na mara chache wanasheria km Lissu, Marando na
Prof.Safari. Kwanini Zitto umekuwa mbali sana na matamko haya ya CHADEMA
ukiwa kama Naibu Katibu mkuu? (Naamini hutojibu ni mgawanyo wa kazi)
10) Unafikiri CHADEMA uliyoikuta mwanzo ndiyo hii ya sasa au kuna
mabadiliko? Kama kuna mabadiliko ni yepi na unafanya nini kufanya
CHADEMA iwe kama ambavyo ulitaka iwe?
11) Unafikiri namna CHADEMA inavyoendesha siasa zake kuna
uwezekano wa kushika dola mapema (2015)? Kama ndiyo kwanini na kama
hapana unafikiri mabadiliko gani yanatakiwa kufanyika kuelekea 2015?
12) CCM wanadai kuwa nyinyi CHADEMA hamna presidential materials, una kauli gani juu ya hili?
13) Una muono gani kuhusu upinzani nchini na nini nafasi ya upinzani
hasa CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ukilinganisha na chama
tawala CCM?
ZITTO: Nitajibu tena kidogo kidogo maana hii peke yake ina maswali 13.
1.Nini kipaumbele chako cha sasa kama mwanachama wa CHADEMA?
- Kutumikia chama chetu kwa nafasi nilizonazo.
Natumia nafasi yangu ya Ubunge na Uwaziri kivuli kuhakikisha kuwa chama
kinapata taswira chanya mbele ya jamii, Na kinaleta mabadiliko ambayo
chama tawala, yaani CCM, kinashindwa kuwafikishia wananchi. Utaona
kwamba, kama unafuatilia Bunge, hakuna mkutano wa Bunge unaopita bila
hoja mahususi inayojenga taswira chanya ya chama.
Ni bahati mbaya sana kuwa hatutumii baadhi ya mafanikio yetu Bungeni
kwenye ulingo wa siasa ma hivyo kuwaacha CCM wanachukua credits.
Kwa mfano, ni kwanini mafanikio ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri
Mkuu hatujayafanyia kazi ya kisiasa? Ingawa hatukufanikiwa kumtoa Waziri
Mkuu lakini tuliilazimisha Serikali kufanya mabadiliko. Kikwete alisema
ni upepo tu, lakini upepo huu ulikuwa na joto kali ukamshinda na
tukaacha yeye achukue credit kwa kazi yetu ya uwajibikaji.
Hoja ya juzi ya Mheshimiwa Halima Mdee kuhusu Ardhi inabidi kuifanya ni
ajenda ya kisiasa. Hoja ya Mkonge tulikwenda Tanga na ilikuwa na
mafanikio makubwa sana. Hoja ya Mabilioni ya Uswiss nayo tunaiachia
wanaisemea watu wa CCM kuififiza. Historia inatuonyesha kuwa hoja zote
tulizozitumia vizuri nje ya Bunge zilijenga taswira nzuri ya chama ie
Buzwagi na EPA. We ignore this at our own peril
2.Mkuu, ni kweli kuwa CHADEMA ni chama cha kidini/kikabila? Na
kama ni kweli, tatizo hilo lishughulikiwe vipi? Kama si kweli, unaweza
kuueleza umma wa watanzania una kauli gani juu ya mitizamo hii dhidi ya
chama chenu?
- Chadema ni chama cha kitaifa. Kingekuwa chama cha
kidini au kikabila kingefutwa. Katika uongozi wa Chadema unapata watu
toka mikoa na kabila mbali mbali, pia watu toka dini mbali mbali.
Diversity hii haipatikani katika vyama vingi humu nchini. Nadhani
mtazamo huu unapandikizwa na watu ambao hawakipendi chama chetu na wanao
ona chama kama threat kwa maslahi yao binafsi.
Pia sisi kama chama tunapaswa kuwa makini sana, hasa viongozi
tunapofanya kazi zetu ili kutothibitisha taswira hii mbaya dhidi ya
chama chetu. Baadhi ya wanachama wa CHADEMA ndio mabingwa wa kueneza
jambo hili. CCM nao humo humo wanapandikiza mbegu za chuki. Unakuta
Waziri wa CCM anamwita Mbunge wa CHADEMA na kumwambia, fulani bwana
mdini sana. Mwangalieni. Kiongozi wa CHADEMA anajiona kapata bonge ya
issue na kueneza. Tunachinjwa na CCM kwa upuuzi wetu. Kwa ujinga wetu
wenyewe. Chama chetu kimesambaa nchi nzima na viongozi wake ni wa dini
zote na makabila yote.
3.Mh. Zitto, unaizungumziaje demokrasia ndani ya chama chako katika chaguzi, teuzi na kupanga safu za uongozi?
CHADEMA ina demokrasia ya aina yake na wanachama tunaridhika nayo.
The Party deploys for or against your wishes and every member must
oblige a just deployment. Tuna utaratibu mzuri sana wa kujieleza na
kutetea hoja zetu ndani ya chama, na baada ya watu wote kukubaliana tuna
hakukusha tunasimama wote kwa kauli moja sehem zote tunapo wakilisha
chama. Sio katika kupanga safu za uongozi tu, ni sehem zote za uongozi
wa chama.
4.Kwanini CHADEMA haiwatumii viongozi wa Mikoa na Wilaya na badala
yake inatuma watu toka makao makuu hata kwa mambo madogo madogo ambayo
yangemalizwa na uongozi wa ngazi husika?
Huo mtazamo unaweza kutokana na kulinganisha Chadema na vyama
vingine. Ieleweke kua Chadema ni chama tofauti na kina utaratibu wake.
Katika chama chetu Viongozi wa mikoa na wa wilaya wana majukumu yao, na
makao makuu pia yana majukumu yake.
Inaweza kutokea mara kwa mara hizi level mbili zishirikiane katika
kutekeleza kazi za chama. Hata hivo, tunaendelea kujenga chama kama
taasisi, hivyo tunaendelea kujenga uwezo wa viongozi wetu wa mikoa na
wilaya ili waweze kumudu majukumu mengi zaidi na kuwaachia wenye kukaa
makao makuu kuhusika zaidi na strategies za chama.
5.Mh Zitto, unazizungumziaje harakati za M4C na athari (impact)
yake kisiasa na kijamii? Chama kimeweka taratibu gani nzuri za malezi
kwa wanachama wapya wanaojiunga kwenye M4C, kama bado, huku si kusuka
kamba inayoungua?
Kwa sababu jina lake liko wazi kabisa, M4C ni moja ya operesheni
inayo fanikisha watanzania kujiunga katika chama huku wakijua kabisa kua
malengo ni kuleta mabadiliko chanya.
Impact yake kwa jamii ni kubwa sababu inawaweka wanachama wenyewe kua
vyanzo vya mabadiliko. Baada ya kujiunga, ni obvious kua Chama kinatoa
mafunzo kwa wanachama wake wapya na hivyo kuwalea kuwa makada wazuri.
Hii sio opresheni ya kwanza ya Chama, na haitakua ya mwisho.
M4C sio chama ndani ya chama, M4C ni operesheni ya kujenga chama na kuleta mabadiliko nchini.
6.Inadaiwa hushiriki kikamilifu M4C, ni kweli? Nini kauli yako dhidi ya tuhuma hizi?
Ninashiriki sana kazi za kujenga chama. Nimeshiriki sana
operesheni mbalimbali za chama. Nitaendelea kushiriki nikiwa mwanachama
na kiongozi wa chama.
Halikadhalika wengine tunashughulika zaidi katika kuwakilisha chama
Bungeni na mikakati mengine ya kuhimarisha chama, ila tukipata nafasi
tunajiunga pia katika kazi za kujenga chama. Mikutano yetu ya chama
tunagawana maeneo.
Mimi, kwa mfano kwenye M4C nimepangiwa mkoa wa Manayara na Singida
nikiwa na Tundu Lissu na Christina Lissu na Rose Kamili. Mtakumbuka
mwanzo mwa mwaka nilifanya ziara Tanga bila viongozi wenzangu.
Mtakumbuka nilikwenda Marekani kufungua tawi la chama kule. Nimefanya
mikutano Iringa, Hanang nk. Nimeshiriki kampeni za udiwani maeneo
mbalimbali nchini. Siwezi kuonekana kila mkoa kila wakati. Pia
ninapangiwa kazi.
7.Je, utaratibu wa kupita mikoani katika kutafuta nafasi ya
kugombea uenyekiti kama ilivyokuwa wakati wa Mbowe unafaa au CHADEMA
irudi katika utaratibu kama wa CCM?
Hatujawahi kufanya utaratibu unaosema isipokuwa kwenye Urais mwaka
2005. Hatujarejea tena utaratibu huo. Mfumo wowote ambao unapanua
demokrasia ya chama ni bora zaidi katika kuimarisha chama. Chama
kinakomaa kwa wanachama kushindana kwenye chaguzi za ndani. Natumai
uchaguzi mkuu ujao wa chama utakuwa na wagombea wengi zaidi ili
wanachama wapate uchaguzi wa kweli. Sipendi chaguzi za kupita bila
kupingwa katika chama kinachotaka kujenga demokrasia ya nchi.
8.Mheshimiwa Zitto Viongozi/CHADEMA imekuwa mstari wa mbele
kufichua ufisadi. Kuna taarifa kuwa kuna mwanachama wenu katafuna fedha
za M4C, ni kweli? Kama ni kweli, ameshughulikiwaje? Kama
hajashughulikiwa, ni kwanini mko kimya?
Nasikia suala hili hapa, tupeni ushahidi na tutachukua hatua mara moja.
9.Zitto wewe ni naibu katibu mkuu wa CHADEMA, Mara nyingi matamko
ya chama yametolewa na Katibu, Mwenyekiti, Mnyika (tangu kabla hajawa
msemaji) na mara chache wanasheria km Lissu, Marando na Prof.Safari.
Kwanini Zitto umekuwa mbali sana na matamko haya ya CHADEMA ukiwa kama
Naibu Katibu mkuu? (Naamini hutojibu ni mgawanyo wa kazi)
Naibu Katibu Mkuu sio msemaji wa chama. Katika kujibu suala la
demokrasia katika chama nilisema kuwa kuna utaratibu wa kujadili hoja
mbali mbali ndani kwa ndani, yakiwemo matamko ya chama.
Katibu mkuu wa CHADEMA anapotoa matamko ya chama anatoa yale
yaliyojadiliwa na wanachama wote, nikiwemo mimi, hivyo kuwakilisha maoni
yangu pia. Sidhani kama kuna umuhimu wa kuifanya kazi hiyo wakati
nimeridhika kua maoni yangu yanawakilishwa kupitia utaratibu wa chama.
10.Unafikiri CHADEMA uliyoikuta mwanzo ndiyo hii ya sasa au kuna
mabadiliko? Kama kuna mabadiliko ni yepi na unafanya nini kufanya
CHADEMA iwe kama ambavyo ulitaka iwe?
CHADEMA ni chama kinachokua kwa kasi sana, na kadiri kinavyokua
kinabadilika positively. Moja ya mabadiliko hayo ni idadi ya wanachama,
nyingine ni kuweza kushika Uongozi wa Upinzani Bungeni, nafasi ambayo
ilikua ya
CUF nilipo ingia chama. Chama hivi sasa kipo kila mahala.
Nakumbuka mwaka 2005 tulikwenda Mafinga kuhutubia tukapata watu 20 tu
kwenye mkutano. Leo tunaombwa kwenda huko. Chama kina influence maamuzi
ya nchi hivi sasa. Hayo yote ni mabadiliko makubwa na mazuri, na
ninafurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya chama changu.
11.Unafikiri namna CHADEMA inavyoendesha siasa zake kuna uwezekano
wa kushika dola mapema (2015)? Kama ndiyo kwanini na kama hapana
unafikiri mabadiliko gani yanatakiwa kufanyika kuelekea 2015?
Sina mashaka na hili. Nitafafanua zaidi baadaye
12.CCM wanadai kuwa nyinyi CHADEMA hamna presidential materials, una kauli gani juu ya hili?
Kweli unategemea kuwa chama tawala kinaweza kukisifu chama cha
upinzani kwa kuwa na presidential material? Mimi ni Presidential
material kwa mfano.
Nina Uwezo, Uadilifu na Uzalendo wa kuweza kuwa Amiri Jeshi Mkuu. Dkt.
Slaa ni Presidential Material. Mbowe ni Presidential material. Kitila
Mkumbo ni Presidential material. Wapo wengi sana ndani ya CHADEMA wenye
sifa za kuwa Marais. Sina mashaka kabisa hilo.
13.Una muono gani kuhusu upinzani nchini na nini nafasi ya upinzani
hasa CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ukilinganisha na
chama tawala CCM?
Ili Tanzania iwe salama ni lazima CCM ishindwe uchaguzi. CCM
ikishinda tena mwaka 2015 itavunja sana moyo wa wananchi na wengine
wanaweza kukata tama. Lakini pia CCM imechoka na haina nguvu za kutosha
kukabiliana na changamoto za nchi hivi sasa.
Njia pekee ya kuisadia CCM iweze kujipanga upya ni yenyewe kondoka
madarakani. CHADEMA ina nafasi kubwa sana ya kushinda na kuongoza dola.
Muhimu chama kijipange na kuonekana kama chama kilichotayari kushika
dola. Tuyatende tunayoyasema na tujiimarishe zaidi.