Unordered List

Pages

Tuesday, January 1, 2013

MWANAJESHI ALIYEPIGA PICHA NA LEMA ATOROKA

>>> JESHI LAENDELEA KUMSAKA



JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema askari anayedaiwa kuwa jeshi hilo aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ametoroka.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema jana kwamba pamoja na hatua yake ya kutoroka, jeshi litaendelea kumsaka kwa udi na uvumba ili kumhoji na kujiridhisha kama kweli ni mwanajeshi wake kabla ya kumchukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kifungu cha 147 cha Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya 1977.
“Huyu kijana inasemekana alishawahi kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lakini wakati tunaendelea na uchunguzi alitoroka katika nyumba aliyokuwa amepanga bila ya taarifa kwa baba mwenye nyumba,” alisema Kanali Mgawe na kuongeza:
“Askari huyo alikuwa anaishi katika nyumba ya kupanga mita chache karibu na Kituo cha Polisi cha Simanjiro, Arusha na alikuwa akijishirikisha na ulinzi shirikishi.”
Alipoulizwa jina la askari huyo, Kanali Mgawe alijibu: “Yeye alikuwa anafahamika mtaani hapo kwa jina la kamanda.”
Hata hivyo, Kanali Mgawe alisema jeshi hilo litahakikisha linatoa ripoti kamili kwa umma baada ya kumkamata na uchunguzi kukamilika ili kuondoa utata uliogubika suala hilo.
Alipoulizwa kama kuna tofauti gani kati ya mwanajeshi kuingia kwenye mikutano ya wanasiasa na wale wanaofanya kazi za kisiasa kama wakuu wa wilaya na mikoa, Kanali Mgawe alijibu:” Wanajeshi wanaofanya kazi za U-DC au RC, wanaruhusiwa kisheria.”
Alifafanua kuwa iwapo mwanajeshi atateuliwa kufanya kazi katika taasisi yeyote ya Serikali nje ya jeshi, atatakiwa kuvua magwanda ya jeshi na kufanya kazi hiyo mpaka atakapomaliza muda wake na baada ya hapo ataruhusiwa kurejea jeshini.
“Kuna kitu kinaitwa ‘secondment.’ Mwanajeshi anaruhusiwa kufanya shughuli zozote nje ya jeshi iwapo atahitajika kufanya hivyo. Ila kwa masharti ya kuvua magwanda, hivyo wananchi wasishangae kuwaona baadhi ya askari wetu ni wakuu wa wilaya na mikoa na baadaye kurudi jeshini kuendelea na majukumu yao,” alisema Kanali Mgawe na kuongeza:
“Askari akiwa katika majukumu yake mapya, atafanya kazi zote atakazopewa zikiwamo za kisiasa kama ilivyo kwa wakuu wa wilaya na mikoa, lakini akirudi jeshini, anarudi kuwa askari mwenye utii na kufuata kanuni za jeshi zisizofungamana na siasa.”

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Blogger